HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 06, 2013

Kwa nini Siasa itishie Maisha ya Wahanga wa Mafuriko ya Maji Kilosa?

Na Bryceson Mathias
 
HIVI karibuni Viongozi wa Wahanga wa Mafuriko ya Maji Kilosa, wameilalamikia Serikali Kuu kwamba, kuna watu wasiowafahamu wanaotishia maisha yao, ati kutokana na wao kuhoji ahadi ya Rais Jakaya Kikwete kuwapatia makazi ya Kudumu.
 
Wamedai, watu hao wanaowatishia maisha inawezekana wamepata maagizo kwa baadhi ya Viongozi wa Siasa na Serikali wilayani Kilosa ambapo wamesema, hivi sasa wanalala usingi wa Mang;amung’amu wakihofu wanaweza kufanyiwa jambo baya.
 
Bila kuwataja viongozi wanaowatuhumu wilayani humo kwa Majina, wamedai kutokana na Tabia mbaya iliyokithiri nchi ya kutekwa watu na kutupwa porini, Kung’olewa Kucha, Macho, Kujeruhiwa na Kuuawa ovyo hata kwa Mabomu, na wao wana hofu.
 
Wameongeza kwamba, wao wanashangazwa sana na tabia ya baadhi ya Vionozi wa Serikali na Wanasiasa Uchwara, wanaojaribu kuwazuia wananchi wanaohoji haki zao kwa Rais waliyemchagua na kumpa Dhamana ahudumie, hasa akiwa aliwapa ahadi.
 
“Mwandishi; Kimsingi nchini kwetu ukitaka ukitaka Ubaya, Dai haki yako! Utanyanyaswa, Utapuuzwa, utaonewa, na ikibidi utaumizwa na kuuawa bila hata sababu ya msingi, kisa tuu umedai haki yako! Jamani tutafika kweli?
 
“Ni kweli nchi yetu viongozi wanainadi ni nchi ya Kisiwa cha Amani, lakini Amani ipi kama baadhi ya Viongozi wanalichafua Jina la Amani ya nchi yetu kiasi kuipaka Jina Vurugu na Maafa?alisema mmoja wao.
 
Alhamisi ya Julai 4, ilifahamika Viongozi wa Wahanga hao, Mathey Gervas, na Nashon Salehe, wameikuwa wakibishiwa Hodi nyumbani mwao na wanapokaidi  kufungua wanatishiwa maisha na watu wasiowafahamu, kisa kikiwa ni wao kuhoji ahadi ya Rais Kikwete kuwapatia makazi ya Kudumu.
 
Wakizungumza na gazeti hili [4.6.2013] toka Mafichoni Wahanga hao walisema, kilichosababisha waanze kufuatwa fuatwa na kutishiwa maisha, ni baada ya taarifa za malalamiko yao kuripotiwa na Radio ya Jamii Kilosa,
 
Waliotishiwa maisha ni pamoja na Mwenyekiti Salehe anayeongoza maeneo yote ya walioathirika, Mazuria, Kimamba na Kondoa, na alipohojiwa toka alipojificha alikiri kufuatwa fuatwa usiku nyumbani kwake na watu asiowafahamu, huku wakimtishia maisha kwa nini anahojihoji ahadi ya Rais, ‘Lini atawapatia makazi ya kudumu’.
 
“Wanakuja usiku nyumbani kunibishia hodi, na ninapotaka wajitambulishe ni akina nani, huwa hawataki kujitambulisha zaidi ya kunitaka nifungue mlango, na nikisema sifungui wananitishia kuwa maisha yako yamo hatarini, wewe na mwenzako Geervas”.alisema Salehe huku akisisitiza, “ukitaka ubaya nchini dai haki yako”!
 
Salehe alisema, watu hao wanadai maswali tunayohoji kuhusu ahadi ya Rais Kikwete kwa Wahanga wa Kilosa si ya kwetu, wanahofu labda tumefundishwa na baadhi ya wanasiasa wanaokinzana nao au pengine tumefundishwa na wanaharakati walio kinyume nao.
 
Aidha gazeti lilimtafuta Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Eliasi Tarimo, ambaye pia ni  Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama, ambapo alipigiwa simu ya kiganjani 0787976111 ili kutoa ufafanuzi wa madai hayo, awali alisema yuko kwenye kikao apigiwe baadaye! Alipoandikiwa Ujumbe mfupi sms alikanusha (kwa njia ya ujumbe) akisema,
 
“Hakuna ukweli wowote katika madai hayo. Naomba nikuulize. Serikali inaweza kutisha wananchi wanapodai haki yao? Naomba uje ofisini upate ukweli kuhusu suala la Wahanga na hatua ambayoSerikali imeshachukua ikiwa ni pamoja na kuwaandalia Viwanja vya Kujenga”.
 
Wilaya ya Kilosa na hasa Ruaha, imekuwa na Mvutano mkubwa baina ya Vyama Vikuu vya siasa nchini, Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
 
Msuguano huo ulipelekea kutofanyika Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Ruaha, ambapo baadhi ya Viongozi wa Chadema Ruaha akiwemo Isack Maliwa, Salehe Nyiko na George Kongo, wapo ndani kutokana na kugombea Uenyekiti wa Serikali ya Kijiji.
 
Adha na adhabu ya Mafuriko waliyopata wananchi hao, kimsingi inatosha kuwa kilio na maombolezo makubwa kwao, pengine haikutegemewa bado wananchi hao wakidai haki yao wafikiwe mahali pa kutishiwa maisha yao! Mbona hiyo itakuwa adhabu nyingine tena mbaya?
 
Aug 17, 2012, Katibu Mkuu wa CHADEMA Dr. Willbrod Slaa alimtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutoa taarifa ya Michango iliyotolewa na nchi marafiki,Makampuni,Taasis na watu binafsi kwa wahanga wa Mafuriko ya Kilosa.
 
Pia Slaa alisema Serikali itoe taarifa ya Michango iliyotolewa kwa Wahanga wa Mafuriko ya Dar es salaam na Mabomu ya Mbagala. Slaa aliyasema hayo katika Wilaya ya Kilosa baada ya kuwatembelea Waathirika wa Mafuriko ya Kilosa katika Makambi yao.
 
Mvutano huo, pia ulisabaisha Uharibifu wa Mali na Vurugu za kufunga barabara ya Dar-es-salaam Mbeya mara kadhaa, jambo ambalo wanasiasa uchwara walio waroho wa kung’ang’ania Madaraka na Vyeo, kwa mara nyingine wameonekana kuwa vyanzo vya Vurugu inayotesa na kupoteza maisha ya watu bila sababu.
 
 

No comments:

Post a Comment

Pages