HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 06, 2013

WAKULIMA WASHAURIWA KUVUNA MAJI YA MVUA

Na Ferdinand Shayo,Arusha

Wakulima wameshauriwa kujenga tabia ya kuvuna maji ya mvua na kuyatumia katika shughuli za umwagiliaji hasa katika kipindi  ambacho mvua ni chache na  haziendani na kalenda ya wakulima.
Kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi  ambayo  yamekuwa yakipelekea kukosekana kwa mvua za kutosha na uharibifu wa mazingira nao umetajwa kuwa sababu ya tatizo hilo.

Hali hiyo imekuwa ikipelekea wakulima kupata mazao kidogo ama kutovuna kabisa jambo ambalo limekuwa likisababisha baadhi ya maeneo nchini kuwa hatarini kukubwa na baa la njaa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika mafunzo yanayolenga matumizi ya muongozo kabambe wa umwagiliaji kwa wataaalamu wa kilimo katika mikoa ya kanda ya kaskazini na kati  yaliyofanyika jijini hapa, Afisa Kilimo Mkuu  Bwana Amana Mbowe kutoka Ofisi ya umwagiliaji kanda ya Kilimanjaro  amesema kuwa ni vyema wakulima wakajenga tabia ya kuvuna maji ya mvua na kuyatumia hasa kwa njia ya kujenga mabwawa na kuyahifadhi.

Vile vile amependekeza njia nyingine ya kutumia maji ya ardhini kwa kuchimba visima virefu na vifupi ambavyo vitawasaidia  kulima na kupata mazao mengi badala ya kutegemea mvua ambazo ni chache na haziji kwa wakati zinapohitajika.

Bwana Mbowe amesema kuwa serikali kwa kutambua umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji tayari imeanzisha mpango wa muongozo kabambe wa umwagiliaji  kitaifa ambao uko katika utekelezaji ,na wameweza kuanzisha mabwawa sehemu za Muhenza na skimu ya Mombo.

“Timu ya kuwezesha umwagiliaji (DIDT) District  Irrigation Development Team ndiyo inapeleka mafunzo kuhusu umwagiliaji kwa wakulima ikishirikiana  na wataalamu wa kanda” Alisema Mbowe
Amewataka wakulima kufanya shughuli za umwagiliaji katika utaratibu unaoeleweka ili ziweze kuwa endelevu.

“Umwagiliaji  una gharama ,fedha zinazotakiwa hazifiki kwa wakati na kwa kiasi kinachotakiwa na hiyo ndio changamoto kubwa inayoikabili miradi mingi ya umwagiliaji hapa nchini” Alisema Afisa huyo

No comments:

Post a Comment

Pages