HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 30, 2014

UDA yatoa msaada wa shilingi milioni 15 kwa kanisa la Mt. Rita

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirila la Usafiri (UDA) Bw. Simon Bulenganija (kushoto) akikabidhi hundi yenye thamani ya shilingi milioni 15 kwa Paroko Msaidizi wa Kigango cha kanisa la Mavurunza, Padri Xavery Kassase (kulia) kusaidia mradi wa ujenzi wa nyumba ya mapadri wakati wa harambee iliyofanyika katika Kigango cha Kanisa la Mtakatifu Rita hivi karibuni.
Paroko Msaidizi wa Kigango cha Kanisa la Mavurunza, Padri Xavery Kassase(kulia) akionyesha hundi ya shilingi milioni 15 zilizotolewa na  Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) kwa kigango cha Kanisa la Mtakatifu Rita jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Mchango huo wa kampuni ulitolewa kusaidia ujenzi wa nyumba ya mapadri kanisani hapo. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirila la Usafiri (UDA) Bw. Simon Bulenganija.

Na Mwandishi Wetu   

MAENDELEO ya kijamii na kiuchumi yataweza kupatikana endapo tu kila mtu ataweza kutoa mchango wake kuwasaidia wale wanaohitaji msaada ili kubadilisha maisha yao na kuwa wachangiaji wakubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Bw. Simon Bulenganija wakati wa harambee ya kusaidia ujenzi wa nyumba ya mapadri katika Kigango cha kanisa la Mtakatifu Rita lililopo Kimara jijini Dar es Salaam, ambapo UDA ilichangia shilingi milioni 15.

“Watanzania wasisubiri mpaka makampuni makubwa yajitokeze na kutusaidia kubadilisha hali zetu za kiuchumi na mfumo wetu wa maisha. Mabadiliko yataweza kufikiwa tu endapo kila mmoja wetu ataweza kuchangia kwa nafasi yake kikamilifu. Makampuni yote makubwa na madogo na watu binafsi wenye uwezo wa kusaidia, wawashike mkono wale wanaohitaji msaada ili tuweze kuendelea pamoja,” alisema.

Bw. Simon Bulenganija alisema kuwa kampuni yake imekuwa ikijihusisha na shughuli mbali mbali za kijamii ikiwa ni jitihada madhubuti zinazolenga katika upatikanaji wa maendeleo miongoni mwa watanzania wote.

Alisema kuwa shilingi milioni 15 zilizotolewa na UDA zitasaidia kwa kiasi kikubwa kupiga jeki maendeleo ya kanisa hilo hususani katika ujenzi wa nyumba ya mapadri na baadae kuendelea na mradi wa ujenzi wa kanisa jipya.

“Japokuwa bado kampuni yetu ni kampuni changa ya kitanzania, tumeunda programu yetu ya shughuli za kijamii katika namna ya kwamba shughuli tunazojihusisha nazo, zitasaidia katika kutekeleza ajenda yetu yenye kaulimbiu “ukuaji wa kampuni yetu uwe sambamba na ukuaji wa kiuchumi wa jamii yetu”. Hii pia ni njia pekee ya kurudisha sehemu ya pato letu kwa jamii,” alisema Bw. Bulenganija.

Naye, Bw. Frederick Msumali, Mwenyekiti wa Kigango cha Mtakatifu Rita, aliipongeza kampuni hiyo kwa mchango wake na ushiriki wa Mkurugenzi wa UDA wakati wa shughuli hiyo ya harambee ambayo iliwezesha kanisa hilo kukusanya zaidi ya shilingi milioni 60 zitakazotumika katika mradi huo.

“Tungependa kwa kiasi kikubwa kutoa shukrani zetu kwa mchango uliotolewa na UDA.  Msaada huu kwa kiasi kikubwa utasaidia kupiga jeki mradi wetu wa ujenzi wa nyumba ya mapadri na baadae kuendelea na ujenzi wa kanisa jipya utakaofanyika karibu na kanisa hili la sasa.

“Lakini pia, tunaishukuru UDA kama kampuni na Bw. Bulenganija mwenyewe kwa kuwa mgeni wetu rasmi. Mfano huu unahitaji kuigwa na makampuni mengine nchini,” alisema Bw. Msumali.

No comments:

Post a Comment

Pages