HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 30, 2014

TASWIRA YA ELIMU TANZANIA: Wanafunzi wanasomea nje kwenye miti na kukalia mawe na magogo ya miti, wanaathirika kifaya na kielimu

 Wanafunzi wa Shule ya Kinyambwiga A na B iliyopo Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara wakiwa wamekaa kwenye mawe na magogo ya miti kutokana na shule hizo kutokuwa na vyumba vya madarasa na madawati. (Picha na Ahmed Makongo)
 Wanafunzi wa Shule ya Kinyambwiga A na B wakiwa wamekaa kwenye mawe na magogo ya miti kutokana na shule hizo kutokuwa na vyumba vya madasa na madawati.
 Wanafunzi wa Shule ya Kinyambwiga A na B wakiwa wamekaa kwenye mawe na magogo ya miti kutokana na shule hizo kutokuwa na vyumba vya madasa na madawati.
Wanafunzi wa Shule ya Kinyambwiga A na B wakiwa wamekaa kwenye mawe na magogo ya miti kutokana na shule hizo kutokuwa na vyumba vya madasa na madawati. 

Na Ahmed Makongo, Bunda 
 
WANAFUNZI zaidi ya 300 wa shule za msingi za Kinyambwiga A na B, zilizoko Katika Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, wanaosomea nje kwenye miti wakiwa wamekalia mawe na magogo ya miti, wamesema kuwa wanaathirika sana kiafya na kielimu, kutokana na kupigwa baridi, kunyeshewa mvua, kuchomwa na jua na kukaa kwenye mavumbi.

Kutokana na kukosa vyumba vya madarasa, ambapo mbao za kuwafundishia zimepigiliwa kwenye miti, huku wao wakiwa wamekaa kwenye mawe na kwenye magogo ya miti kwa kukosa madawati, walisema kuwa wanaathirika sana ki-afya na ki-elimu kutokana na hali hiyo.

Wanafunzi zaidi ya 130 wanaosomea nje kwenye miti ambayo imegeuzwa kama vyumba vya madarasa ni wa shule ya msingi Kinyambwiga A, ambao ni wa darasa la pili na tano, waliliambia gazei hili kuwa wanaathirika sana na hivyo wanaomba kuondolewa kero hiyo, ili waweze kupata elimu inayostahili kama wanafunzi wengine walioko kwenye shule zenye ubora.

Nao wanafunzi wa shule ya msingi Kinyambwiga B ambao ni wa madarasa ya pili, tano na sita zaidi ya 180, walisema kuwa wao pia wanaathirika na hali hiyo ya kusomea  nje na kukaa kwenye  mawe na kwenye magogo ya miti.

Wanafunzi wa shule hizo zote kwa ujumla walisema kuwa wanaathirika sana kiafya na kielimu kutokana na mazingira wanayosomea.

Wanafunzi hao waliwaomba wazazi, wananchi na serikali kwa ujumla, kuwaondolea kero hiyo, Ili waweze kusomea Katika mazingira yanayofaa ili waweze kupata elimu inayostahili kama walivyo wanafunzi waosomea kwenye vyumba vya madarasa na kukaa kwenye madawati.

“Hali hii ya kusomea nje na kukaa kwenye mawe na magogo ya miti kwa ujumla sisi tunaathirika sana kielimu na pia kiafya, maana tunapigwa baridi wakati wa asubuhi, tunanyeshewa mvua wakati zinapokuja, tunachomwa na jua wakiti wa mchana na tunaathirika kiafya kwa kukaa kwenye ya mavumbi” walipaza sauti zao  wanafunzi hao wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hizi.

Baadhi ya walimu wa shule hizo wakiwemo walimu wakuu, walisema kuwa kutokana na hali hiyo wamekuwa wakifundisha Katika mazingira magumu, hali ambayo inawafanya watoto kutokuelewa vyema, ikiwa ni pamoja na kutokuwa na miandiko mizuri.

“Hata hawafanyi vizuri kwa  kutokuandika vizuri, pia sisi walimu hata hali ya ufundishaji inakuwa Katika mazingira magumu” alisema mwalimu Mussa Lubeleli wa shule ya msingi Kinyambwiga A.

Afisa elimu wa shule za msingi katika Wilaya ya Bunda, Jeshi Pembe, alithibitisha wanafunzi hao kusomea nje kwa sababu ya kutokuwa na vyumba vya madarasa na kukaa kwenye mawe na kwenye magogo ya miti kwa kukosa madawati.

Pembe alisema kuwa hali hiyo inasababishwa na wananchi wa kijiji hicho kutokuwa tayari kuchangia nguvyu zao kwa kuleta viashiria ili madarasa yaweze kujengwa na kutengeneza madawati.

Wadau wa elimu wakiwemo waandishi wa habari katika Wilaya ya Bunda, walisema kuwa hii ni changamoto kubwa kwa shule hiyo, ambayo wakazi wake ni wafugaji na wakulima ambao wamekuwa wakizalisha mazao mengi ya pamba na mtama, huku wakiwa na mamia ya mifugo hususani ng’ombe, mbuzi na kondoo.

Walisema kuwa iwapo wakazi wa kijiji hicho wakiwa tayari kujitoa na kuchangia nguvu zao, ikiwa ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya hiyo, ambayo uchumi wake unatokana na kilimo, madini, mifugo na uvuvi, shule za Wilaya hiyo kamwe haziwezi kukosa vyumba vya madarasa, madawati, nyumba za walimu na nyingine kufungwa kwa kukosa matundu ya vyoo. 

Hivi karibuni mwandishi wa habari hizi alishuhudia shule ya msingi Machimweru, ambayo pia iko pembezoni, baadhi ya wanafunzi wakiwa wanasomea  nje kwenye miti, huku  idadi kubwa ya wanafunzi wake wakiwa wanasoma wakiwa wamekaa kwenye mawe kwa kukosa madawati.

No comments:

Post a Comment

Pages