HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 15, 2014

WATATU WAFARIKI DUNIA KWA KUCHOMWA MOTO

DAR ES SALAAM, Tanzania

WATU watatu wamefariki Dunia jijini Dar es Salaam baada ya kupigwa na kuchomwa moto na  wananchi kwa tuhuma za wizi wa piki piki.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala  Mary Nzuki,  alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 6:30 mchana huko maeneo ya Zingiziwa kata ya Chanika.

Nzuki  alisema watu watatu wanaume wasiofahamika  wenye umri kati ya miaka 25 na 30  wameuawa baada ya kushambuliwa na wananchi waliojichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga kwa fimbo na mawe hadi kufa kisha kuwachoma moto kwa tuhuma za kumpora  Zablon Kerekaro (18) mkazi wa Rubakaya aliyekuwa akiendesha  piki piki yenye namba za usajili T – 376 CWX  aina ya Fekon yenye rangi nyekundu.

Alisema  Kerekaro majira ya saa sita mchana alitoka Chanika ili ampeleke Videte maeneo ya  Zingiziwa, wakiwa njiani abiria huyo alimuomba asimame ili ajisaidie baada ya kusimama ghafla abiria huyo alimkaba.

Kwa mujibu wa Nzuki  baada ya tukio hilo, walitokea watu wengine wawili na  kumdhibiti kumfunga kamba mikononi  na miguuni kisha kumlaza  kichakani huku wakimpiga ngumi na mateke, hatimaye waliondoka na pikipiki hiyo.

Kwa mujibu wa Nzuki, wakati  tukio hilo,linaendelea dereva mmoja wa bodaboda ambaye bado hajafahamika alikuwa akilishuhudia tukio hilo, ndipo alianza kuwafuatilia wezi hao huku akifanya mawasiliano na madereva wenzake  hatimaye kundi kubwa la waendesha pikipiki likaanza kuwafuatilia na kuwakuta wamejificha kwenye kichaka wakiwa na pikipiki walizopora.

Nzuki alisema waendesha bobaboda hao walianza kuwapiga hadi kuwauwa  na kuwachoma moto sehemu kubwa za miili yao  hali iliyosababisha kushindwa kutambuliwa miili yao.

Nzuki alibainisha kuwa sehemu ya tukio zilikutwa hirizi tatu nyekundu zilizozungushiwa shanga zinazosadikiwa kupatikana kwa wezi hao kabla hawajauwawa.Miili ya maiti hizo zimehifadhiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

No comments:

Post a Comment

Pages