HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 13, 2014

AZAM, YANGA HAPATOSHI LEO

Kocha Msaidizi wa Azam, Kalimangonga Ongara akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuhusu pambano lao na Yanga la Ngao ya Hisani litakalofanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja Masoko wa Shirika la Bima ya Taifa (NIC), Elisante Maleko na Meneja Biashara wa TFF, Peter Simon.

Na Mwandishi Wetu

Ligi Kuu Tanzania bara itakayoanza Septemba 20, inazinduliwa leo katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kwa mechi ya Ngao ya Jamii kati ya bingwa mtetezi, Azam FC na Yanga iliyomaliza msimu uliopita nafasi ya pili.


Akizungumzia mechi hiyo, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Kally Ongara, alisema kwao Ngao ya Jamii, ni kombe muhimu ambalo wanalisaka  kuingia katika orodha ya mataji yao kabatini, hivyo wanaipa uzito.

“Hii ni mechi iliyobeba taswira yetu ya msimu ujao kwani kupitia mechi hii, tutaweza kujua mwelekeo wa kikosi chetu katika mbio za kutetea taji la Ligi Kuu. Tulichofanya mwaka jana, kila timu inaweza. Lakini kutetea, ndio jambo gumu kwetu,” alisema Ongara.

Alisema, wanawaheshimu Yanga kama moja ya timu kongwe nchini, lakini kwa suala la kupigania ushindi, wamejipanga kuhakikisha wanaondoka na ushindi na kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza katika historia yao.

Ongara aliyasema hayo jana alipomwakilisha bosi wake, Joseph Omog katika mkutano huo wa makocha uliofanyika Ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuelekea mechi hiyo ambapo hata hivyo upande wa Yanga hawakufika.

Kabla ya mkutano huo, Azam FC ilitumia ukurasa wake wa Facebook kuandika kauli ya Omog akisema ni mechi muhimu, hivyo vijana wake watapambana kuibuka na ushindi kuyafikia malengo yao.
“Ni mechi muhimu! Kocha Mkuu wa Azam FC, Joseph Omog, ameutaja mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga kuwa ni muhimu. Omog amesema ni muhimu kwa timu yake kushinda mchezo huo, ili kuimarisha morali ya timu kabla ya kuanza kwa ligi,” ukurasa huo ulisomeka. 

Kupitia ukurasa huo, Omog raia Cameroon, aliongeza kuwa amewapa wachezaji wake kila kitu kitakachowawezesha kushinda mechi hiyo, hivyo kazi imebaki kwao kushinda na kuleta furaha kwa timu hiyo.
Azam inacheza mechi hiyo kwa mwaka wa tatu mfululizo, ambapo miaka miwili ilicheza kama makamu bingwa na mara zote ilipoteza dhidi ya mabingwa Simba na Yanga, wakati leo inacheza kama bingwa, hivyo kubebwa na historia ya Ngao ya Jamii. 

Kwa upande wa vikosi, wakati Yanga ikitarajia kuwakosa Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Andrey Coutinho walio na majeruhi, Azam watashuka dimbani bila nahodha wao John Bocco ‘Adebayor’ na Waziri Salum ambao ni majeruhi.

Kwa upande wake Meneja Biashara wa TFF, Peter Simon, alisema kuwa maandalizi ya mechi hiyo yamekamilika na tayari wamepokea maombi mbalimbali ya mgawo wa asilimia 10 ya mapato kwa taassisi za kijamii.

“Tumepokea maombi kutoka Chama cha Wasioona Tanzania, Chama cha Walemavu Tanzania (Chawata) na Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS). Na baada ya mechi tutaona ni kwa namna gani tutawasaidia katika maombi yao,” alisema Simon.

Yanga wao wametumia tovuti kuandika kuwa kikosi chao kinajivunia rekodi nzuri katika mechi za Ngao ya Jamii, na watashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 katika mechi hiyo msimu uliopo, kwa bao la Salum Telela ‘Essien.’

Kwa mujibu wa tovuti hiyo, Maximo atakayeiongoza Yanga mara ya pili katika dimba la Taifa, amesema vijana wake wapo katika hali nzuri jambo ambalo linampa wigo mpana wa kikosi kuchagua nani amtumie katika mchezo huo.

Hadi sasa Maximo ameiongoza Yanga katika mechi nne za kirafiki na kufanikiwa kushinda yote; dhidi ya Chipukizi FC (2-0); dhidi ya Shangani FC (2-0); dhidi ya KMKM (1-0) na 1-0 dhidi ya Thika United ya Kenya.

Katika mazoezi ya mwisho yaliyofanyika jana asubuhi Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola, nyota pekee aliyeshindwa kufanya mazoezi, ni Jerson Tegete, anayesumbuliwa na nyonga
Kuhusu Mbrazil Coutinho, alifanya mazoezi mepesi chini ya daktari Dk. Suphian Juma.

No comments:

Post a Comment

Pages