HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 02, 2014

Kifo cha Ntwina chatikisa Mbeya

Na Christopher Nyenyembe, Chunya

MAELFU ya wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) juzi walijitokeza kwa wingi kumzika, Paulo Ntwina (60) aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo la Songwe (CCM) na kuhamia Chadema mwaka 2010.

Mazishi ya Ntwina aliyekuwa tegemeo kubwa kwa wakazi wa wilaya ya Chunya hususani katika jimbo la Songwe yalifanyika majira ya saa 8.30 katika kijiji cha Galula kwenye makaburi ya kanisa la Roman Katoliki mahali alikozaliwa.

Marehemu Ntwina aliamua kugombea ubunge mwaka 2010 baada ya kujiunga na Chadema lakini jina lake lilienguliwa dakika za mwisho kwa madai kuwa alichelewa kuwasilisha fomu za kugombea na kusababisha mgombea wa CCM,Philipo Mulugo apite bila upinzani.

Habari za kifo cha Ntwina aliyefia jijini Dar es salaam ghafla septemba 26 zilitanda kwa kasi katika wilaya hiyo na vitongoji vyake na hivyo kuwavuta makada wa CCM  wanaowania ubunge katika jimbo la Songwe na Lupa kwenye uchaguzi mkuu mwakani walijitokeza na wafuasi wao kwenye mazishi hayo.

Tukio la msiba liligeuka na kuchomoza  hali ya kisiasa baada ya wafuasi wa Chadema na waonyesha nia kadhaa wa chama hicho waliofanikisha kuushikilia kwa hadhi na heshima kubwa msiba wa Ntwina ambaye bila kujua mauti alijiandaa pia kugombea ubunge mwaka 2015. 

Tanzania Daima ilishuhudia makada wa CCM wakihaha huku na kule kwenye msiba huo uliozingirwa na makundi hasimu ya siasa za Chunya waliofika na wapambe wao,baadhi wakionyesha kujinadi na kutamka wazi kuwa ni wagombea watarajiwa.

Akielezea hali hiyo mdogo wa marehemu,George Ntwina alisema kuwa familia ya Ntwina imefarijika kwa kiasi kikubwa jinsi wananchi walivyoweza kujitokeza na kumzika kwa heshima kubwa kaka yao bila kuathiri shughuli za mazishi.

“Kaka Paulo alikuwa na nia ya kugombea ubunge mwaka 2014 kupitia Chadema,alianza kujiandaa kushinda na hakika amefariki huku akiwa anakubalika kwa kiwango cha juu,lakini Mungu amemuita katika safari yake ya milele,nina imani tutapata mbunge mzuri mwakani” alisema mdogo wa marehemu.

Miongoni mwa waombolezaji waliojitokeza katika msiba huo alikuwepo,Njelu Kasaka aliyewahi kuwa mbunge wa Chunya kwa tiketi ya CCM ,amehamia Chadema na ametangaza nia ya kugombea ubunge jimbo la Lupa mwaka 2015.

Wengine waliotajwa na walikuwepo kwenye msiba huo kuwa wameonyesha nia ya kugombea ni Conrad Mamboleo Mwashambwa(CCM),Regnard Msomba(CCM) na Wolfgang Wanga(Chadema) hao wote wanawania jimbo la Songwe.

Kutoka jimbo la Lupa waliokuwepo msibani na kutajwa kuwa wanawania kiti hicho ili kumuondoa Mbunge wa sasa Victor Mwambalaswa ni Noel Chiwanga(CCM) aliyewahi kuwa mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Chunya na Kasaka(Chadema).

Akielezea hali ya msiba huo na pilikapilika za kisiasa,Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Chunya, Kapala Chakupewa Makelele ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo alisema amefarijika kuona jinsi wakazi wa jimbo hilo walivyojitokeza kumzika Ntwina na huo ndio ushirikiano unaopaswa kuendelezwa.

Kwa mujibu wa taarifa za familia ya Ntwina ilielezwa kuwa marehemu ameacha mke mmoja, Stella Paulo na watoto watatu.

No comments:

Post a Comment

Pages