HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 25, 2014

MAONI YA MSOMAJI KUHUSU MAPENDEKEZO YA KUZUIA AJALI ZA BARABARANI

Mimi ni dereva na pia ni Mwalimu wa madereva “Drivers  Instructor ”. Napenda kutoa maoni  yangu   na mapendekezo kuhusu ajali barabarani kama ifuatavyo:-

Nimefanya uchunguzi kwa muda  wa miaka mitatu kwa madereva tofauti, wa malori makubwa , mabasi makubwa na madogo (daladala), tax pick up za kukodi, malaori ya mchanga, madereva wa  Serikali, madereva wa Waheshimiwa  Wabunge na bajaji.  Kwa makundi yote haya ukiondoa Madereva wa Serikali kinachowafanya madereva hawa kuendesha magari bila kujijali wao wenyewe , abiria na watembea kwa miguu kwa kuendesha mwendo kasi bila ya kujiwekea tahadhari ya chochote barabarani.

Madereva karibu asilimia 92 hawana ajira ya kudumu wala mikataba inayoainisha malipo na maslahi yao, hivyo malipo yao ni kutokana na safari wanaozifanya na idadi ya tripu, hali hiyo inawalazimu madereva kama wa bus wakimbie ili ajitahidi azipite gari zilizomtangulia bila kujali madhara yanayoweza kumkuta endapo atapata ajali. Unaweza kukuta madereva wengine mfukoni hawana hata shilingi  elfu kumi (10,000/=) ambayo inaweza kuwa ya thadhari ya kumuona dokta kwa hatua ya huduma ya kwanza endapo atapata ajali. Hali hii inasikitisha sana kulingana na thamani ya gari analoliendesha , uhakika wa kama baba mwenye majukumu haupo.

Angalieni tunaoenda mjini upande wa daladala ikitokea tu dereva kutofautiana na konda anavua nguo palepale barabarani (Uniform) na kumtupia kondakta wa gari ambazo kondakta ana mamlaka makubwa juu ya gari hilo. 

Pia angalieni baadhi ya madereva  wa waheshimiwa wabunge nao nimeshuhudia mara mbili wakiwasilisha malalamiko yao kuhusu maslah yao kutokakana na hela ya malipo yao kupewa wabunge wawalipe na baadhi ya wabunge kuwadhulumu, sasa kwa hali hii utamuona dereva anaendesha barabarani kumbe anawaza.

 Pia mimi binafsi sikubaliani na kauli za kuwashutumu askari wa usalama barabarani (traffics) kuwa ndio wanawaachia madereva , askari hao wanafanya kazi yao ipasavyo na ndiyo maana gari ikipewa ishara ya kuwa mbele kuna “ Traffics” utashangaa anapunguza mwendokasi, pia ikumbukwe hawa askari baadhi yao tunaishi nao mitaani, utakuta dereva anafanya kosa na anakwenda kumuomba askari ili tu ahalalishe makosa yake, lakini hatuthubutu kumshauri dereva chochote kulingana na makosa tunayoyaona anafanya, mfano: pale Ubungo mataa kukiwa hakuna askari wa usalama  barabarani dakika tano nyingi magari yanafungana na hayatembei.

 Sasa napenda nitoe mapendekezo yangu ili kutatua au kupunguza ajali kama ifuatavyo:-
Katika utafiti wangu nimengundua ni mambo mawili yakifanyika yatasaidia kupunguza ajali.
     i.        ELIMU
Ninaiomba serikali ifanye jitihada  za makusudi itafute hata wafadhili ili kuwezesha vyuo vya mafunzo ya udereva NIT na VETA vipunguze ada ifike hata elfu hamsini (50,000/=) ili idadi kubwa ya madereva waweza kumudu gharama maana wengi wa madereva wamekaa miaka mingi bila mafunzo “training ” za mara kwa mara ambazo zitamuwezesha kujitambua, kujiamini na kujielewa  majukumu aliyo nayo, naamini serikali inaweza kusaidia hilo kama ilivyowezakuchukua hatua za tahadhari kutokana na mlipuko wa Ebola kwa kuhakikisha vifaa vinapatikana haraka na ajali za barabarani tuchukulie kama janga kutokana na kusababisha vifo na ulemavu kwa watu wengi, mfano kwa wastani bus moja lina watu 65 ambapo ikitokea ajali , vifo na majeruhi yanayosababisha ulemavu  hutokea  serikali ifanye jitihada za kutoa elimu endelevu kwa madereva.

   ii.        MIKATABA YA KAZI
Naiomba serikali itafute njia ya kudumu ya kuweka  mikataba kwa madereva binafsi wa magari kama vile mabasi, daladala , malori na kadhalika, ambayo itaanisha mishahara , matibabu  na marupurupu mengine , baadhi ya viongozi wetu wametembelea nchi za nje wameona madereva walivyo na nidhamu  kuheshimu sheria za barabarani na hata kuheshimu watembea kwa miguu. Naamini madereva binafsi wakipata Elimu ya Udereva na mikataba  au ajira ya kudumu, marupurupu yao yaainishwe na ikiwezekana mishahara  waikute benki na wawe na uwezo au wa kukopa benki hakika ajali zitapungua.

Kwa ufupi haya ni mawazo yangu na mapendekezo.

Natanguliza shukrani za dhati


YUNUS SEIF KANDUGUDA
   ................................

No comments:

Post a Comment

Pages