HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 19, 2014

MAHAKAMA KUU KANDA YA DAR ES SALAAM YAWAHUKUMU WATU SITA KUNYONGWA HADI KUFA

Na Mwandishi Wetu

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewahukumu kunyongwa hadi kufa washitakiwa sita katika kesi ya mauji ya  polisi na mafanyakazi wa NMB tawi la Wami Morogoro na kuiba kiasi cha shilingi milioni 150.

Hukumu hiyo imetolewa leo na Jaji Projest Rugazia ambaye alianza kuisoma kuanzia saa 10:02 asubuhi hadi saa 12:20 mchana, huku akitumia lugha ya Kiswahili kusoma hukumu hiyo kwa taratibu ili kila mtu aelewe.

Washtakiwa hao ambao wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa ni Mashaka Pastory, John Mndasha, Martine Mndasha, Haji Kiweru,  Wycliff Imbora na Rashidi Abdikadir, huku wengine nane wakiachiwa huru.

Jaji Rugazia alisema aliwatia hatiani washtakiwa hao na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa, kufuatia ushahidi ulitolewa na mashahidi 29 wa upande wa mashtaka pamoja na vielelezo 78 vilivyowasilishwa mahakamani hapo na ushahidi wa utetezi.

“Maungamo ya washtakiwa, ushahidi wa kitaalam na utambuzi wa washtakiwa kutambuliwa eneo la tukio inaonesha wazi walikuwa na nia ya kujaribu kupora Sh 150 milioni mali ya benki ya NMB zilizokuwa zikisafirishwa kutoka  Dar es Salaam kwenda  Morogoro tawi la Wami.” Alisema Jaji Rugazia.

Jaji Rugazia alieleza kwamba, katika siku hiyo ya huzuni Aprili 20, 2006 mashitakiwa hao walilivamia gari kwa lengo la kupora lakini  bila ya kuwa na huruma yoyote walilimiminia risasi na kuwaua  D 6866 Konstebo Abdallah Marwa na mfanyakazi wa NMB tawi la Wami Morogoro, Ernest Manyonyi.

Akizidi kufafanua kwa hali ya ustadi na utaratibu, Jaji huyo alisema tukio hilo la kusikitisha lilifanyika nyakati za saa 6:30 mchana, eneo la Ubungo Mataa jijini Dar es Salaam kwenye makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nujoma.

Akiendelea kusoma hukumu hiyo, Jaji Rugazia alisema miongoni mwa kundi hilo la majambazi ambao walikuwa 14 kuna baadhi yao wameokoka na adhabu ya kunyongwa hadi kifo baada ya kuona hawana hatia.

Aliwataja watu hao, huku baadhi ya ndugu na jamaa waliokuwa ndani ya mahakama wakibubujikwa na machozi kuwa ni Rashid Lemblisi, Philipo Mushi, Yassin Juma,Hamisi Daud.

Wengine ni MT 77754 Nazareth Amurike, MT 76162 Emmanuel Lameck, James Chamangwana na Hussein Idd baada ya kuwaona hawana hatia katika kesi hiyo.

Kwa upande wa washtakiwa, Jackson Issawangu aliyekuwa mshtakiwa wa sita katika kesi hiyo na Mussa Mustafa aliyekuwa mshtakiwa wa 10 waliachiwa huru awali baada ya mahakama hiyo kuwaona kuwa hawana kesi ya kujibu.

 Hadi wanaachiwa huru jana, washtakiwa hao walikuwa wamekwisha kaa rumande kwa muda wa zaidi ya miaka 8.

Awali, wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, mahakama hiyo ilitupilia mbali vielelezo muhimu vya ushahidi katika kesi hiyo ya mauaji ikiwemo ripoti saba, kati ya nane za uchunguzi wa silaha zilizotumika katika mauaji hayo.

Baada ya Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Godfrey Luhamba,  Mtaalam wa milipuko kuiomba mahakama hiyo ipokee ripoti hizo kama vielelezo vya ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo. 

Mawakili wa upande wa utetezi wakiongozwa na Richard Rweyongeza, walipinga ripoti hizo kupokewa, wakidai kuwa ziliwasilishwa kinyume cha sheria kwa kuwa hazikusomwa kwa washtakiwa wakati wa kuhamisha kesi hiyo kutoka Mahakama ya Kisutu kwenda Mahakama Kuu.

 Katika uamuzi wake, Jaji  Rugazia alikubaliana na utetezi kuwa kwa kuwa ripoti hizo hazikuwahi kusomwa kwa washtakiwa, basi mahakama hiyo haiwezi kuzipokea kwa kuwa uwasilishwaji wake ulikuwa ni kinyume sheria.

Pia alikataa hoja za upande wa mashtaka kutaka mahakama iamuru washtakiwa hao warudishwe tena mahakama ya chini (Kisutu), wakasomewe ripoti hizo, au iamuru upande wa mashtaka uwapatia upande wa utetezi wapate muda wa kuzipitia na kisha kuendelea.
Alisema kuwa mapendekezo hayo ya upande wa mashtaka hayaungwi mkono na kifungu chochote cha sheria.

Hata hivyo mahakama hiyo ilipokea ripoti moja tu ambayo ndio iliyosomwa kwa washtakiwa katika mahakama ya chini, ambayo inabainisha kuwa maganda mawili ya risasi, yaliyopatikana katika eneo ya tukio yalitoka kwenye bastola mojawapo, zilizokamatwa kwa washtakiwa.

Ripoti nyingine zilizokataliwa zinahusu bastola nane, na SMG 5 na Shortgun moja, ambazo zote zilikamatwa kwa washtakiwa.

No comments:

Post a Comment

Pages