HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 25, 2014

Mnyika azibana Dawasco, Dawasa kero ya maji

Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), amezitaka Mamlaka ya Maji safi na Maji taka (Dawasa), na Kampuni ya Maji safi na Maji taka (Dawasco), Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, kueleza ni lini mgawo wa maji utapungua jijini.

Mnyika alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akitoa taarifa ya hali ya mgawo wa maji inavyoendelea katika jimbo hilo.

Mbunge huyo alitoa kauli hiyo baada ya kugundua kuna mitaa ambayo mgawo wa maji haujarejea katika hali ya kawaida, ndiyo maana akazitaka Dawasa na Dawasco watoe taarifa kwa umma kwamba matatizo katika maeneo hayo yaliyobaki yatamalizika lini.

Aliyataja maeneo ambayo yameathirika kuwa ni Jimbo la Ubungo na Segerea jijini Dar es Salaam na Kibaha mkoani Pwani, yanayopata maji kutoka mtambo wa Ruvu Juu.

Mnyika alisema kuna baadhi ya maeneo katika jimbo lake hali ya maji imeanza kurejea katika hali ya kawaida, ambayo ni Kata ya Kibamba, Kwembe, Msigani, Mbezi Luis, Kimara, Saranga, Ubungo na Makuburi.
 
Hata hivyo, alisema katika kata hizo ipo mitaa ambayo mgawo haujarejea katika hali ya kawaida, hivyo kuzitaka Dawasa na Dawasco zijitokeze kutoa taarifa kwa umma ni lini hasa matatizo katika maeneo yaliyobaki yatamalizika.

“Aidha, namtaka Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe, kujitokeza hadharani ili atoe taarifa kwa umma kuhusu ripoti ya uchunguzi juu ya kujirudia rudia kwa matatizo ya maji katika mtambo wa Ruvu Juu,” alisema.

Mnyika alisema matatizo hayo yameathiri wananchi wa Ubungo na Segerea jijini Dar es Salaam na Kibaha mkoani Pwani, hususan katika maeneo ambayo yanahudumiwa na Dawasa.

“Suala hili nililiombea muongozo wa Spika bungeni, Waziri Maghembe akajibu kuwa imeundwa kamati ya uchunguzi... lakini katika mawasiliano yangu na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Amos Makalla, alinieleza kuwa uchunguzi umekamilika lakini hakutoa taarifa hiyo bungeni,” alisema na kuongeza kuwa, 

kwa maelezo ya Makalla, taarifa hiyo ni kwamba ripoti hiyo ya kamati ya uchunguzi tayari imekwisha kukabidhiwa wizarani kwa ajili ya kuichambua.


“Hivyo ni muda wa kutosha umepita, nawataka Maghembe na Makalla waiweke taarifa hiyo hadharani kupitia kwa waandishi wa habari na tovuti ya wizara,” alisema Mnyika na kuongeza kuwa, pia waeleze hatua walizochukua ikiwemo kuwachukulia hatua wanaofanya biashara haramu ya maji na kuhujumu miundombinu ya maji, hali ambayo inawaathiri wananchi.
               

No comments:

Post a Comment

Pages