HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 19, 2014

PROF. MAGHEMBE AZINDUA RIPOTI YA UTENDAJI WA MAMLAKA YA MAJI NA USAFI WA MAZINGIRA ZA MIKOA NA MIRADI YA KITAIFA

 WAZIRI wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe (katikati) akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzindua ripoti ya Utendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira za Mikoa na Miradi ya Kitaifa.

 Na Mwandishi Wetu
 
WAZIRI wa Maji Prof. Jumanne Maghembe amesema Serikali inadaiwa bilioni 15 na mamlaka za maji nchini.
Hayo aliyasema jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa ripoti ya utendaji wa mamlaka za maji za mikoa na miradi ya maji kitaifa.
Alisema ukubwa wa deni hilo limekuwa likipunguza uwezo na ufanisi wa kazi katika mamlaka hizo ikiwemo Dawasco na Dawasa.
"Watu wadogo wadogo ndio ambao wanalipa vizuri bili zao za maji, lakini mashirika ya serikali hayalipi kabisa, hususani vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Dawasco peke yake inaidai serikali bilioni 10.5, ucheleweshaji wa ulipaji wa deni hili pia unapunguza uwezo wa mamlaka za maji kununua madawa ya kusafishia maji," alisema.
Maghembe alisema wale wote wanaodaiwa wanatakiwa kulipa madeni hayo, kwani hali hiyo inahatarisha usalama wa upatikanaji wa maji safi kwa wananchi.
Aidha alisema moja ya mashirika vinara kwa kupoteza maji ni Dawasco na Dawasa, ambao hupoteza kwa asilimia 56, hivyo amewataka wabadilike katika utendaji wao wa kazi na upotevu huo usizidi asilimia 20.
"Mikoa mingine ambayo pia ni vinara kwa upotevu wa maji ni Mwanza, Bukoba, Arusha. Sasa nataka kuona mabadiliko makubwa na kila mamlaka ionyeshe inakidhi viwango vya kimataifa kwa kutoa maji safi na salama," alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Simon Sayore, alisema ripoti imebainisha kuwa kama ilivyokuwa mwaka 2012/13, miundo mbinu kwa ajili ya uzalishaji wa maji bado haitoshelezi mahitaji katika maeneo mengi yanayohudumiwa na mamlaka za maji.
Vile vile alisema ripoti inaonyesha kuwa upotevu wa maji bado ni tatizo, hivyo wanaamini kwa sehemu kubwa mamlaka za maji zina uwezo wa kuchukua hatua ili kupunguza tatizo hilo, kwani pamoja na kuhitajika fedha za kukabili nalo, vile vile uwajibikaji makini wa wafanyakazi wa mamlaka hizo unahitajika.

No comments:

Post a Comment

Pages