HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 22, 2014

RAIS KIKWETE ATENGUA UTEUZI WA WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI, PROF. ANNA TIBAIJUKA KUTOKANA NA KASHFA YA ESCROW

Rais Jakaya Kikwete akiwapungia mkono wazee wa mkoa wa Dar es Salaam alipokuwa akiwasili kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam kuzungumza na wazee kuhusu mambo mbalimbali pamoja na sakata la Escrow. (Picha na Francis Dande)
Rais Kikwete akizungumza jijini Dar es Salaam kuhusu sakata la Escrow.
 Rais Jakaya Kikwete akifafanua jambo kuhusu sakata la Escrow.
Viongozi mbalimbali wakifuatilia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete.
 Rais Kikwete akitafakari jambo.
Viongozi wa Kamati ya Amani inayounganisha viongozi wa dini zote wakiwa katika ukumbi wa Diamond Jubilee wakifuatilia hotuba ya Rais Kikwete.
Baadhi ya wazee wakifuarahia maamuzi ya Rais Kikwete ya kumfuta kazi Waziri Anna Tibaijuka baada ya kutengua uteuzi wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Prof. Anna Tibaijuka baada ya kukiuka Maadili ya Utumishi wa Umma baada ya kupokea Sh. bilioni 1.6 fedha za Escrow.


 Tanzania Daima, Desemba 23


RAIS Jakaya Kikwete ameshindwa kuchukua uamuzi mgumu dhidi ya maazimio ya Bunge kuhusu sakata la uchotwaji wa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Tegeta Escrow na badala yake ameishia kumtoa kafara Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka.

Mbali na kumtoa kafara Prof. Tibaijuka, Rais Kikwete amewaweka kiporo Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, akisema uchunguzi dhidi yake unaendelea na Katibu Mkuu wake, Eliachim Maswi, aliyesema kuwa taratibu za utumishi wa umma zinaendelea.

Katika hatua ya kushangaza, Rais Kikwete alionyesha kupingana kiaina na ripoti ya uchunguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akisema kuwa fedha hizo zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow si za umma kama Bunge na wananchi walivyoaminishwa.

Rais pia ameonyesha hatua hafifu ya serikali yake katika kutekeleza maazimio manane ya Bunge kuhusu sakata hilo, ambapo alipinga mitambo ya IPTL kutaifishwa na kumilikishwa kwa Tanesco, akisema kuwa uamuzi huo utawatisha wawekezaji.

Akihutubia taifa jana kupitia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, rais alisema kuwa kabla ya kufikia uamuzi huo, walikaa na Prof. Tibaijuka na kumuuliza maswali mbalimbali, ikiwa ni pamoja na fedha hizo kuingia katika akaunti yake binafsi badala ya shule aliyoeleza.

“Kuna sababu za maadili katika hili, hivi kweli fedha nyingi kiasi hicho zinaingia katika akaunti yako wala hushtuki, hili haliwezekani hata zile mana zinazoshuka haiwezi kuwa hivyo.

“Tumezungumza naye na kumshauri atuachie nafasi tumuweke mtu mwingine,” alisema Rais Kikwete huku akionyesha kusitasita, hatua iliyowafanya baadhi ya wazee hao kupiga kelele za kuzomea wakidhani anataka kumlinda.

Kabala ya kutangaza kumvua uwaziri Prof. Tibaijuka, Rais Kikwete alisema serikali inawajibika na watumishi wa umma kwa kusimama katika maadili ya viongozi na kwamba yeyote aliyekiuka maadili hayo atashughulikiwa ipasavyo.

Kuhusu Waziri Muhongo, Kikwete alisema kiongozi huyo wamemuweka kiporo kwa kuwa yupo katika uchunguzi maalumu na kwamba ukikamilika watafanya uamuzi ili watu waendelee na shughuli nyingine.

Katika hotuba yake ya zaidi ya saa mbili, Rais Kikwete alionekana kuunga mkono ushauri wa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, akisema kuwa fedha za Escrow hazikuwa za umma, japo kuna kodi ya serikali ya sh. bilioni 21 ambayo haikulipwa.

Alisema kuwa vyombo husika vitafanya uchunguzi na ikithibitika kodi hiyo lazima italipwa.

Akizungumzia maazimio manane ya Bunge kwa kutoa ufafanuzi wa kila kipengele na namna kitakavyotekelezwa, alisema kuwa serikali inayaunga mkono kwa kiasi kikubwa na kwamba jambo muhimu ni kuchukua tahadhari katika uamuzi wowote utakaofikiwa.

Alisema kwa sasa serikali inachunguza kama Kampuni ya PAP iliponunua hisa kutoka Pipelink ilikuwa inajua kama kuna zuio la hisa hizo kuuzwa na kama ilikuwa inajua itakuwa ilishiriki katika udanganyifu, hivyo kuchukuliwa hatua.

Azimio la kwanza alilotolea maelezo ni lile la kuitaka serikali iangalie uwezekano wa kununua au kuitaifisha mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za shirika hilo, akisema kuwa suala hilo ni gumu kwani linaweza kuwa na athari kwa nchi na kuwatisha wawekezaji.

Alisema kwa sasa kazi kubwa iliyopo ni kuwarejesha wafadhili na kuwaondoa katika dhana kuwa Tanzania inatekeleza sera ya ujamaa kwa kutaifisha mali za wawekezaji.

Kuhusu uwazi wa mikataba mbalimbali, Rais Kikwete alisema serikali itakaa na Bunge kuangalia namna bora ya kufanya kwa ajili ya kutunza siri za wawekezaji zisivuje kwa wafanyabiashara wenzao.

Azimio la tatu la kutaka Jeshi la Polisi na vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua stahiki kwa waliohusika na uchotwaji wa fedha za Escrow, alisema uchunguzi unaendelea kwa hatua mbali mbali.

Kuhusu wabunge wenye nyadhifa kwenye kamati za Bunge kuondolewa mamlaka hayo, Andrew Chenge (Kamati ya Bajeti), William Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala) na Victor Mwambalaswa, alisema hilo ni suala la Bunge lenyewe. 

Azimio namba tano kwa mujibu wa Rais Kikwete ni lile lililotaka kuundwa kwa tume ya kijaji kwa ajili ya kuwachunguza majaji Prof. Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Jaji Aloysius Mujulizi, waliopokea mgawo wa fedha kutoka kwa Rugemalira. 

Katika hili, Rais Kikwete alisema utaratibu wa kuwashughulikia unanzia katika Mahakama na kwamba jukumu hilo amemuachia Jaji Mkuu chini ya Tume ya Majaji kuchunguza na kutoa ushauri kwa mamlaka ya uteuzi.

Kuhusu Benki ya Stanbic kutangazwa kuwa benki inayotakatisha fedha haramu, Rais Kikwete, alisema tayari mamlaka husika za kifedha zinachunguza suala hilo.

Akiongelea kuvunjwa kwa Bodi ya Tanesco, Rais Kikwete alisema bodi hiyo imemaliza muda wake na kwamba muda wowote atatangaza uongozi mpya.
Uamuzi wa Rais Kikwete, ulipokewa kwa vifijo na nderemo na wananchi wengi huku Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda akigoma kuzungumzia hali hiyo.

Kwa upande wake mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale -Mwiru, alisema kilichofanyika ni uamuzi sahihi, huku Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, akieleza kuwa rais ametekeleza wajibu wake kama Bunge lilivyoshauri.

1 comment:

  1. MUNGU IBARIKI TANZANIA NA UONDOE ROHO YA KIFISADI

    ReplyDelete

Pages