HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 27, 2015

Kitabu cha Dira na Tumaini Jipya Handeni

Mwandishi wa habari za michezo wa gazeti la Bingwa, Dimba na Mtanzania kutoka Kampuni ya New Habari 2006 Ltd, Sharifa Mmasi pichani akisoma kitabu cha Dira na Tumaini Jipya Handeni kilichoandikwa na Kambi Mbwana, ambaye ni Mratibu Mkuu wa Tamasha la Handeni Kwetu linalofanyika kila mwisho wa mwaka wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWANDISHI wa Habari za Michezo ambaye pia ni Mratibu Mkuu wa Tamasha la Utamaduni la Handeni Kwetu, Kambi Mbwana, ameandika kitabu chake kinachojulikana kama ‘Dira na Tumaini Jipya Handeni’, kilichoanza kupatikana mapema wiki hii jijini Dar es Salaam na wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Kitabu hicho kimeelezea kero na changamoto mbalimbali za wananchi wa Handeni, kama vile shida ya maji, elimu na migogoro ya ardhi kwa ajili ya kushirikisha mawazo ya viongozi wa serikali, wadau na wananchi ili kukabiliana na tatizo hilo wilayani humo na mikoa ya jirani ambapo changamoto hizo zinashabihiana kwa kiasi kikubwa.


Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mbwana alisema kwamba kuandika kitabu hicho kuna lengo kubwa la kuelimisha jamii kwa ajili ya kutafuta fursa ya kimaendeleo katika wakati huu ambao wananchi wengi wamekuwa wakilia bila kupata msaada wowote.

“Naijua vizuri wilaya yangu ya Handeni na mkoa wa Tanga kwa ujumla, hivyo nimeamua nitumie kipaji change katika kuandika kitabu hiki ambacho kimeweza kuanika mambo mengi yenye tija kwa serikali na wananchi kwa ujumla, hivyo naomba waniunge mkono kwa kuhakikisha kwamba wanapata kitabu hiki popote kitakapokuwapo.

Kinapatikana kwa bei ndogo mno ya Sh 3500 kwa kuwa sikuwa na lengo la kutajirika kwa kupitia kitabu hiki bali kutoa mawazo yangu na kuelimisha jamii yangu inayonizunguuka, hivyo ni wakatai wa Watanzania wote, bila kusahau wakazi na wananchi wa Handeni kupata nafasi ya kusoma mawazo yangu kwa ajili ya kutafuta namna ya kufika mbali kiuchumi na kiutamaduni, ukizingatia kuwa kitabu kimegusia mambo kadhaa ambayo ni muhimu,” alisema Mbwana.

Kwa mujibu wa Mbwana, maeneo yanapopatikana kitabu hicho kwa jijini Dar es Salaam ni pamoja na ambapo ni Kinondoni Kwa Manyanya, kwenye kituo cha basi kwa muuza magazeti aliyekuwa pembeni ya ghorofa la Mwaulanga, Sinza Kijiweni kwenye studio inayoangaliana na lango la New Habari 2006 Ltd, upande wa wanaokwenda mjini, huku studio hiyo ikiwa karibu na duka la vifaa vya ujenzi. Maeneo mengine ni muuza magazeti wa Kimara Mwisho kwenye kituo cha basi cha wanaokwenda mjini, huku Buguruni kikipatikana katika studio ya upigaji wa picha karibu na Hoteli ya New Popex, Buguruni, jijini Dar es Salaam.

Aidha Mbwana alisema kwa wanaotaka kuwasiliana naye juu ya kitabu hicho cha Dira na Tumaini Jipya Handeni wanaweza kumpata kwa +255 712053949 au barua pepe; kambimbwana@yahoo.com

No comments:

Post a Comment

Pages