HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 16, 2015

CHE MUNDUGWAO AFARIKI DUNIA, KUZIKWA DAR

MWANAMUZIKI wa nyimbo za asili na mtayarishaji wa vipindi vya radio, Chigwele Che Mundugwao, amefariki dunia leo saa moja asubuhi, akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa akitibiwa wakati akishikiliwa na Jeshi la Magereza.

Che Mundugwao (48), alikuwa akiishi gerezani kwa sababu alikuwa akikabiliwa na kesi ya wizi wa Pasi za kusafiria (pasipoti), mali ya serikali tangu aliposhitakiwa rasmi Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Juni 2, 2013 na wenzake.

Kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Samuel Mbwana, alithibitisha kutokea kwa kifo cha Che Mundugwao, na kusema msiba uko Tegeta Azania kwa kaka wa marehemu, na kwamba atazikwa saa 10 alasiri.

“Ni kweli Chemundugwao amefariki na msiba uko Tegeta Azania kwa kaka wa marehemu. Familia na kamati ya mazishi ziko katika majadiliano na hakuna uamuzi uliofikiwa wa makaburi gani atazikiwa, ingawa imekubaliwa azikwe Dar,” alisema Mwana.

Che Mundugwao, Ofisa Manunuzi wa Idara ya Uhamiaji, Shemweta Kilwasha (33), Mhandisi wa Idara ya Zimamoto na Ukoaji, Keneth Pius 39 na mfanyabiashara, Ally Jabir ( 36), walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na jumla ya mashitaka manne likiwemo kosa la wizi wa jumla ya Pasipoti 26.

Katika kesi hiyo, makosa waliyokuwa wakishitakiwa nayo yalikuwa na dhamana kwa mujibu wa Sheria, ingawa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kwa mamlaka aliyonayo, ana haki kuzuia dhamana, mamlaka iliyomlazimu Che Mundugwao kusota mahabusu.

No comments:

Post a Comment

Pages