HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 27, 2015

MALINZI AFUNGUA KOZI YA WAKUFUNZI

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Jamal Malinzi leo amefungua kozi ya walimu wakufunzi wa mpira wa miguu chini inayofanyika katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.

Malinzi amesema kozi hiyo ni muhimu kwa mustakabali wa soka la Tanzania, walimu wakufunzi watasaidia kuwafundisha walimu wengine wa mpira, ili kuweza kufundisha mpira kwa watoto wadogo ambao ndio hazina ya baadae.

Malengo ya TFF ni kuhakikisha timu ya vijana ya U17 inafuzu kwa fainali za Mataifa Afrika 2017 nchini Madagscar, na baadae kuwa na kikosi bora wakati tunapotarajia kuwa wenyeji wa fainali za U17 Afrika mwaka 2019 "alisema Malinzi".

TFF ina program mbili za kuwaandaa vijana wenye umri chini ya miaka 13, 15 kwa kuwaweka kambini na kucheza michezo ya kirafiki mikoani na kufanya ziara katika nchi za Malawi, Zambia, Zimbabwe, Bostwana na Afrika Kusini.

Aidha Malinzi amewaomba walimu wakufunzi kuwa karibu na makocha wa timu za Taifa, na kuwapa ushauri makocha hao ili kuweza kuwasaidia katika kuboresha vikosi vyao na maendeleo ya soka la Tanzania kwa ujumla.

Naye Rais wa CECAFA na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF, Leodgar Tenga alimshukuru Malinzi kwa kuweza kufungua kozi hiyo ambayo inawakutansisha walimu wakufunzi wa mpira miguu kutoka sehemu mbalimbali nchini.

 Akiongea kwa niaba wa walimu wakufunzi, Dr. Mshindo Msolla alisema wanaishukuru TFF kwa kuandaa kozi na kuomba kuendelea kushirikishwa katika mipango mbalimbali ya soka nchini ikiwa ni pamoja na kutambulika kuanzia katika ngazi za juu mpaka katika maeneo waliyopo.

Kozi hiyoiliyoanza leo jumatatu itamalizika Mei 2 mwaka huu, inawajumuisha walimu 18, wenye leseni A, B na C za CAF kutoka mikoa mbalimbali Tanzania bara na Zanzibar.


IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments:

Post a Comment

Pages