HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 27, 2015

Bulaya: Asante kuuhesabu U-DC, uwaziri kama majitaka

Na Bryceson Mathias

AKIHUTUBIA katika mkutano wa hadhara uliofanyikia katika viwanja vya stendi ya zamani mjini Bunda hivi karibuni, aliyekuwa Mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ester Bulaya, baada ya kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alieleza alivyofanya uamuzi mgumu ambao haujafanywa na mtu yeyote, isipokuwa Mtume.

Bulaya alituambia, wakati Chama chake cha zamani cha CCM kilipogundua mikakati yake ya kuhamia Chadema, makada wake chama hicho walimwendea wakimsihi asitoke, bali abakie ili apatiwe ukuu wa wilaya au uwaziri.

Anasema, baada ya kutafakari kwa muda mrefu uhalisia wa maisha ya Watanzania hasa wa vijijini na jinsi ambavyo Serikali ya CCM imekuwa ikiwatendea, aliamua kuachana na ahadi hizo na kujiunga na Chadema kwa kuwa inalenga kuwakomboa Watanzania.

“Ngojeni niwaambie, niliahidiwa ukuu wa wilaya na uwaziri ilimradi tu nisihame CCM. Lakini nikaona yote hayo ni upuuzi, bali cha muhimu ni kuwakomboa Watanzania, nikaachana nayo yote nikaja kujiunga Chadema,” alisema Bulaya.

Kauli ya Bulaya kuikataa rushwa ya U-DC au Uwaziri wa Mlango wa Nyuma na kuufanya kuwa ni upuuzi, ni sawa na Mtume Paulo aliyewaambia Wafilipi, jinsi alivyoona Mwokozi wake Yesu Kristo ni muhimu kwake kuliko kupata faida zake binafsi.

Paulo alisema: “Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu. 
“Ambaye kwa ajili yake, nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nimpate Kristo. 

“Tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani.” Filipi 3:8-9.

Bulaya aliyekulia na kufanya kazi ndani ya CCM, anasema chama hicho hakina sera zozote za kuwakomboa Watanzania badala yake kuna za kuwanufaisha wachache, jambo ambalo yeye na Mbunge mwenzake, James Lembeli, wa Kahama hawakulitaka. 

Hivyo kwa ukweli huo, Bulaya na Lembeli, wamefanya matendo kama aliyofanya Nabii Musa nyakati zile.

Musa alilelewa na kukuzwa na Mfalme Farao, lakini alipoona Wana wa Israel wanateswa, wakifanyishwa kazi ngumu na kudhulumiwa haki yao, alimbadilikia mfalme huyo, hata kama kwake alikula mayai, nyama na mikate yenye siagi.

“‘Bwana akamwambia Musa akisema: “Ingia kwa Farao, ukamwambie, Bwana asema hivi: “Wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia. Tena kama ukikataa kuwapa ruhusa, tazama, nitaipiga mipaka yako yote kwa kuleta vyura; Musa alifanya hivyo bila kujali, mradi awakomboe watu.”

Katika Kutoka 10:1 inasema: “Bwana akamwambia Musa, Ingia wewe kwa Farao; kwa kuwa mimi nimeufanya moyo wake mzito, nipate kuzionyesha ishara zangu hizi kati yao.” Hapa ndipo ninaposema, ujasiri wa Bulaya sio wake binafsi bali kuna mkono na maagizo ya Mungu ndani yake, ili awakomboe Watanzania.

Mimi binafasi, ningependa maamuzi Magumu kama aliyofanya Bulaya na Lembeli, yasiishie tu katika kutambulishwa kwao, bali nilitaka yaende mbali ili, ikiwezekana, wabunge wa upinzani, kuonyesha kwamba wako kwa ajili ya kuwakomboa Watanzania, waongeze kufanya yafuatayo:-

Kwanza, ni rai yangu, endapo Rais Jakaya Kikwete, ataridhia maombi ya Tume ya Utumishi wa Bunge, ya kumlipa kila mbunge mafao ya sh. milioni 238 baada ya Bunge kuvunjwa, basi wawepo wabunge wenye maamuzi magumu ya kuwarejeshea fedha hizo walalahoi kama Bulaya.

Ingawa tayari wananchi na wanaharakati mbalimbali wamekwisha kuonyesha wazi kupinga mpango huu wa wabunge wa kujineemesha. 

Wanaopinga wanasema jamii inakabiliwa na matatizo makubwa, hasa ya ukosefu wa huduma muhimu za kijamii, hivyo si jambo la busara kutumia sh. bilioni 85 kuwalipa wabunge mafao. 

Ni matumaini yangu kwamba, kama wabunge wa upinzani pamoja na wale wenye mapenzi mema na wananchi watawaonea huruma walipa kodi wao na kubeba mzigo mzito migongoni mwao, hasa wakati huu ambao kila kitu kimapanda bei, wananchi watamtazama kwa jicho la tatu.
Mwaka mmoja Mwalimu Nyerere alikubali mshahara wake ukatwe kuchangia maendeleo ya Watanzania, wapo pia baadhi ya watu kama, Edward Moringe Sokoine, waliodiriki hata kukatia risiti fedha walizopewa kwa kazi halali katika nchi hii, ili zirejeshwe kwa umma! Leo watu hao wapo?
Kama watu wa namna hiyo ya Nyerere, Sokoine tunao, basi hao ndio ambao hata wakifanyiwa mizengwe, kama alivyofanyiwa Bulaya na Lembeli, wananchi tutawachukuliwa Fomu za kuwania uongozi, hata kama watakuwa gerezani wamefungwa kwa sababu mbalimbali za kulitetea taifa hili.
Tuseme tisa, lakini 10, mtumishi wa Mungu Yoshua 24:15 katika huduma yake ya kumtumikia Mungu alisema:

“Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao. Lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana.”

Tunataka watu watakaowatumia wananchi wa Tanzania na si matumbo yao. Si watu ambao hata kama ni viongozi wa dini, mfano; wachungaji au masheikh ndani ya Bunge, ambao wanakubali kudanganywa na kufikia kujificha hata kwenye vivuli vya siri,  hata za kusema uongo na kuwadhulumu wananchi.

Watu wa namna hiyo, hawahitajiki tu kwenye Bunge, bali hata kwenye makanisa na misikiti yao, na ikiwezekana wakataliwe hata na familia zao kwa sababu wanaliaibisha taifa, jamii na koo zao.

Nasema hivyo si kwa sababu nataka kuwasema viongozi wa dini katika majukumu yao, lakini kwa siku za hivi karibuni, kuna tatizo lililovifanya vyombo hivyo vipakwe matope na viongozi hao wachache, kwa sababu ya kuacha wajibu wao kwa Mungu na kujiunga na matendo ya kishetani.

Dhambi sasa hivi imepiga hodi mpaka kwenye mimbari za madhehebu hayo, hivyo ukiangalia na kutazama ndani ya misikiti na makanisa, unashangaa kuona watu wanafanya uovu hadi unajiuliza; je, humo ndani kuna viongozi wa dini wenye kukemea au hakuna?

Kimsingi tulitarajia tuone viongozi wa dini wawe wa kwanza kuikemea Serikali, Bunge na Mahakama, hata kabla ya wananchi kuamua kuandamana. 

Kinachoshangaza, kuna wimbi la uovu, na tunapoona watu wanauawa mchana kweupe (albino), lakini wakifikishwa  mahakamani, kesi zinacheleweshwa!
Tunashuhudia Bunge linatunga na kupitisha sheria mbovu, na wakati mwingine kutumia wingi wa watu fulani katika chama kupitisha sheria zisizo na mashiko, ambazo baadaye zitaliangamiza taifa la sasa, kesho na vizazi vijavyo.

Aidha, tumeshuhudia serikali ikiwakumbatia watenda maovu na wengine hivi karibuni pamoja na kuwepo taarifa za ufisadi ulio wazi, lakini wameendelea hata kutetewa kwa maelezo mbalimbali, mfano ni Prof. Sospeter Muhongo, Anna Tibaijuka na wengine katika Tuhuma za Escrow.

Ikifika hapo, ndipo ninaposema: ‘Asante Bulaya kuuhesabu U-DC na uwaziri kama majitaka’.

No comments:

Post a Comment

Pages