HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 27, 2015

Chadema: Magufuli, CCM hawamtangulizi Mungu

 Na Bryceson Mathias, Morogoro

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimempasha na kumjibu mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Pombe Magufuli, kwamba CCM imemtanguliza shetani badala ya Mungu, ndiyo maana inashindwa kukomesha mauaji ya wakulima na wafugaji Mvomero.

Katibu wa Chadema Mvomero, Ramadhani Mrisho, alimnanga Magufuli akisema: “Magufuli alikuwa kwenye Baraza la Mawaziri kwa miaka 10, lakini hakumtanguliza Mungu ili ampe  hekima ya kumshauri Rais Jakaya Kikwete na CCM wakomeshe mauaji hayo na badala yake yanaendelea hadi leo.”

Alisema CCM na Magufuli wanashindwa kuelewa kuwa mgogoro wa wakulima na wafugaji unaosababisha, mauaji katika  bonde la mpunga la Mgongola na Mbigiri na Mabwegere, Kilosa, unasababishwa na Wana-CCM wanaotaka kuhodhi kwa nguvu maeneo ya wakulima, hivyo mchawi hawezi kujiroga mwenyewe.

Hata hivyo Mrisho amemnyooshea Magufuli kidole akisema: “CCM imemtanguliza shetani si kwa mauaji ya wakulima na wafugaji tu, bali hata kwa wakulima wadogo wa miwa Mtibwa, wafanyakazi wa Kiwanda cha Sukari Mtibwa, wanaodhulumiwa haki zao (mishahara na malipo mengine), tangu kiwanda hicho kibinafsishwe, huku serikali na CCM iko kimya, ikikumbatia maovu.

Hivyo Mrisho amedai, kama Magufuli atakuwa rais kwa goli la mkono, basi asipotazama upya, atakuwa akilinda miradi ya wenye uwezo, waliojimilikisha ardhi na kujibinafsisha viwanda, kikiwemo Kiwanda cha Sukari Mtibwa, kinachodhulumu wakulima na wafanyakazi wake, kikidaiwa kuhusishwa na kubebwa na rais mmoja mstaafu.

Kauli ya Chadema Mvomero ilifuatia hotuba ya Magufuli aliyejitambulisha jana mkoani Morogoro ambapo alisema, kuhusu mgogoro na mauaji ya wakulima na wafugaji wilayani Mvomero, wananchi na viongozi, wamtangulize Munngu na kuwa na utu, jambo ambalo Chadema wanasema:

“Mungu katika 1 Timotheo 5:8 anasema: ‘Lakini Mtu yeyote asiyewatunza walio wake (wananchi), yaani wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini…’” 

Hivyo CCM haiwajali watu wake, ni mbaya kuliko wapinzani,  alisema Martha Kimbisa mkazi wa Dumila aliyehudhuria mkutano wa Magufuli.

No comments:

Post a Comment

Pages