HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 16, 2015

Wachimbaji waliofukiwa kwenye mgodi wapatikana wakiwa hai

Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini,  Badra Masoud, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu kupatikana kwa watu 5 walioangukiwa na kifusi kwa siku  41 katika machimbo ya Nyangalata Kahama mkoani Shinyanga. Kulia ni Ofisa habari Idara ya Habari (Maelezo), Jackiline Mrisho. (Picha na Loveness Bernard)
 
Na Jacquiline Mrisho- Maelezo

Wachimbaji wadogo wadogo waliofukiwa  katika mgodi wa Nyangalata ulioko wilayani Kahama wamepatikana wakiwa hai.

Hayo yamesemwa na msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Bi. Badra Masoud alipokua akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuwa wachimbaji hao walikaa kwa muda wa siku 41 kuanzia tarehe 5, oktoba hadi tarehe 15, novemba 2015.

Msemaji huyo amewataja wachimbaji hao waliookolewa wakiwa hai ni Muhangwa Amosi, Joseph Bulule, Chacha Wambura, Msafiri Gerald na Onyiwa Aindo ambao mpaka sasa wako katika Hospital ya wilaya ya Kahama wakiendelea na matibabu kwakua hali zao hazikuwa nzuri.

Aliongeza kuwa mmoja kati ya wachimbaji hao Bw. Musa Supana alifariki dunia siku 15 zilizopita na mwili wake bado haujaonekana hivyo uongozi wa Wilaya kwa kushirikiana na wachimbaji wadogowadogo wanaendelea kuutafuta mwili huo.
Aidha, Bi. Badra aliongeza kuwa wachimbaji hao waliishi maisha ya shida kwa kula magome ya miti na kugawana maji kidogo yaliyokua yakidondoka.

Hata hivyo Wizara inatoa ruzuku na mikopo ili uchimbaji uwe wa kisasa na kutoa wito kwa wachimbaji wachimbe kwa kutumia nyenzo za kisasa na kuwa makini katika  shughuli za uchimbaji.

No comments:

Post a Comment

Pages