HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 01, 2015

Kamal yatoa zawadi ya Krismasi ya viungo mbadala (bandia) kwa walemavu Dar Dar es Salaam

Waziri Mkuu staafu Mizengo Pinda akimkabidhi mguu mbadala Niyo Jonasi Mkazi wa Dar es Salaam ikiwa ni moja kati ya miguu mbadala (bandia) 60 iliyotolewa bure na kampuni ya Kamal Group ya Jijini Dar es Salaam jana. Wengine kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Kamal, Sameer Gupta, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi, Reginald Mengi, Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Donald Mbando na Mwenyekiti wa Kamal Group, Bwana Gagan Gupta. (Picha na Mpigapicha Wetu)


Dar es Salaam, Tanzania

Kampuni ya Kamal Group ya Jijini Dar es Salaam imetoa miguu bandia yenye thamani ya mamia ya mamilioni ya shilingi kwa watu sitini wenye ulemavu wa viungo na kuwafanya washerehekee Krisimasi wakiwa na uwezo wa kutembea tena.
Kampuni hiyo pia imetoa vifaa vya kusaidia kusikia 40 kwa watu wenye usikivu hafifu.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo kwa wahusika, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Bwana Satyam Gupta alisema kampuni yake inaamini kuwa inao wajibu wa kusaidia maendeleo ya jamii inayoizunguka.

“Tunaamini kuwa ni wajibu wetu kusaidia jamii inayotuzunguka….ni wajibu wetu kuleta tabasamu katika nyuso za watu wanaotuzunguka na kuhakikisha kuwa wale wenye ulemavu wa miguu wanaweza kutembea tena,” alisema Bwana Satyam Gupta.

Naye mwenyekiti na mkurugenzi mtendaji wa Kamal Group – kampuni inayojishughulisha na uzalishaji wa nondo zinazokidhi viwango vya kimataifa - Bwana Gagan Gupta alisema kampuni yake amefanikisha zowezi la utengenezaji miguu bandia kwa kutumia wataalam kutoka India.
Wataalamu hao waliletwa nchini ili waweze kutengeneza miguu hiyo hapa hapa nchini kwa kutumia mitambo ya kiwanda cha Kamal kinachotumika kutengenezea nondo.

“Nia yetu ni kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanarudi katika sehemu zao za kazi ili watoe michango yao katika kuijenga Tanzania. Kwa vile tunacho kiwanda chenye zana za kimataifa hapa hapa nchini Tanzania, tulilazimika kuwaleta wataalam tu ili kazi yote waifanyie hapa hapa nchini. Tulichoagiza hapa kutoka nje ya nchi ni malighafi tu,” alisema Bwana Gupta. Wataalam hao ni madktari kutoka katika taasisi ya Bharat Vikas Parishad Viklang Kendra PaldiI, ya nchini India ambao waliongozwa na Bwana Upendra Jani.

Huduma kama hii itawafikia pia watu wenye mahitaji kama hayo wanaoishi Arusha na Mwanza.
Naye mwenyekiti kitaifa wa Chama Cha Walemavu Tanzania (Chawata) Bwana John Paul Mlabu alisema bei ya mguu mmoja bandia kwa sasa inafikia Shilingi milioni nne na hivyo kuwafanya watu wengi washindwe kumudu. Hii inamaanisha kuwa thamani ya miguu bandia 60 ni sawa na Shilingi milioni 240.

“Na ndio maana tunaishukuru sana kampuni ya Kamal kwa msaada huu na tunaomba makampuni mengine nayo yawaige,” alisema.

Alisema Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni mbili wenye uhitaji wa viungo bandia ila kutokana na gharama kuwa kubwa, ni asilimia 20 tu ndio wenye uwezo wa kumudu kuvipata viungo hivyo.

Katika kuhudumia jamii, kampuni ya Kamal pia inaendesha mradi ujulikanao kwa jina Food for Children (Chakula kwa watoto) ambapo kampuni hutoa chakula kwa wanafunzi1,250 kila siku kwa shule za msingi za Nzasa ya Ilala na Kerege ya Bagamoyo. Mradi huo ulioanza mwaka jana utarajia kuwafikia wanafunzi 3000 mwaka 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages