HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 29, 2016

Uchukuzi SC yawa ya tatu, kipa adaka penati

 ·        Kamba wanaume watwaa ubingwa

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

TIMU ya soka ya Uchukuzi SC jana ilitwaa ushindi wa tatu wa mashindano ya Mei Mosi, baada ya kuwashinda Tanesco magoli 3-2 kwa mikwaju ya penati, katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani hapa.

Ushindi wa Uchukuzi SC ulichagizwa na kipa wao mahiri William Barton aliyeweza kudaka penati tatu kati ya tano zilizopigwa na Tanesco.

Baada ya ushindi huo, Barton alimwaga machozi ya furaha, kwani alidaka penati zilizopigwa na kipa mwenzake Hashim Yahya, Khalifa Shekuwe na Abdallah Magubile.

Penati za Uchukuzi SC zilifungwa kwa ufundi stadi na Fidelis Kyangu, Masoud Masoud na Kado Nyoni, wakati waliokosa ni Omary Said ‘Chidi’ na Seleman Kaitaba.

Hatua ya penati ilifuatiwa baada ya timu hizo kutoka suluhu katika dakika 90 za kawaida na kwa mujibu wa sheria za mashindano hayo hakina nyongeza ya dakika 30 na inapigwa mikwaju ya penati moja kwa moja.

Kocha wa Uchukuzi SC, Elutery Muholeli alisema kuwa mchezo ulikuwa na ushindani mkubwa, na wachezaji wake walicheza kwa kujituma, na dhamira yao ilikuwa ni kutwaa ubingwa, lakini bahati haikuwa yao na wamebahatika kutwaa ushindi wa tatu.

Naye kocha wa Tanesco, James Washokera alikiri wachezaji wake kukosa umakini kutokana na kikosi chake kukosa wafungaji, na aliamua kuwatumia viungo zaidi, ili kufunga magoli lakini walishindwa kutokana na kucheza nafasi sio yao.

“Unajua hii timu yetu ilitakiwa kuwa ni kombaini ya Tanesco Tanzania nzima, lakini haikuwa hivyo na badala yake wametoka sehemu chache na nilitarajia ningechagua wafungaji kutoka mikoani, lakini sikupata nafasi hiyo, ila hili tatizo huu ndio mwisho wake na mwakani tutakuja kamili kwani nitahakikisha ninazunguka na kupata wachezaji sehemu zote,” alisema Washokera.

Pia Uchukuzi wanaume wameibuka mabingwa wa mchezo wa kamba baada ya kumaliza ikiwa imejikusanyia pointi 10, na haikuwahi kuvutwa na timu yeyote tangu michuano hiyo ianze.

Nayo CDA ‘Watoto wa nyumbani’ wameshika nafasi ya tatu katika mchezo wa netiboli wakiwa na pointi tatu sawa na Tanesco iliyoshika nafasi ya nne , lakini wanatofautiana kwa magoli ya kufunga na kufungwa, huku TPDC ikiburuza mkia ikiwa haijapata pointi yeyote.
 Abubakar Mwamachi (9) wa Uchukuzi SC akikokota mpira huku mlinzi wa Tanesco Juma Rajabu akiwa ameshika ardhini.
 Omary Kitambo (4) wa Uchukuzi SC akiwania mpira uliopigwa na Stanley Uhagile wa Tanesco. Uchukuzi ilitwaa ushindi wa tatu kwa penati 3-2.
 Kipa Willium Barton wa Uchukuzi SC akikaa tayari kupangua penati ya kipa mwenzake wa Tanesco Hashim Yahya. Uchukuzi ilitwaa ushindi wa tatu kwa penati 3-2.
Wachezaji wa michezo mbalimbali wa timu ya Uchukuzi SC wakishangilia baada ya timu ya soka kutwaa ushindi wa tatu kwa penati 3-2 dhidi ya Tanesco.

No comments:

Post a Comment

Pages