HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 27, 2016

Bagamoyo Half Marathon Julai 24

 Mkurugenzi wa Bagamoyo Historical Marathon, Dominic Mosha akizungumza na waandishi wa habari mjini Bagamoyo mkoani Pwani  jana, wakati wa uzinduzi wa mbio hizo, kwa mwaka 2016, zitakazofanyika Julai 24. Kulia ni Kaimu Katibu Mkuu Riadha Tanzania (RT), Ombeni Zavalla (wa pili kulia) ni Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Ayoub Magimba na Mratibu wa mbio hizo, Dorah Raymond.
 Kaimu Katibu Mkuu Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Ombeni Zavalla (kulia) akizungumza na waandishi wa habari mjini Bagamoyo mkoani Pwani  jana, wakati wa uzinduzi wa mbio za Bagamoyo Historical Marathon 2016, zitakazofanyika Julai 24. Wa (pili kulia) ni Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Ayoub Magimba, Mkurugenzi wa Mbio hizo, Dominic Mosha (wa pili kushoto) na Mratibu wa mbio hizo, Dorah Raymond.

NA MWANDISHI WETU, BAGAMOYO

MBIO za Bagamoyo Historical Half Marathon 2016, zinatarajiwa kufanyika Julai 24 mjini hapa na kushirikisha wanariadha kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Mbio hizo za kila mwaka, zimeandaliwa na Kampuni ya 4Bel kwa lengo la kukuza vipaji vya wanariadha chipukizi kutoka maeneo tofauti.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bagamoyo mkoani Pwani jana, Mkurugenzi wa 4Bel, Dominic Mosha, alisema wamezindua rasmi mashindano hayo ili kuutaarifu umma na kuwakaribisha kushiriki.

"Tumezindua rasmi mashindano, tunaendelea na maandalizi kwa kasi,” alisema Mosha.
Alisema zoezi la usajili na fomu kutolewa kwa ajili ya washiriki litaanza Julai 4, ambapo wanawaalika washiriki kutoka mikoa tofauti wajitokeze kwa wingi.

Alisema lengo lao safari hii ni kufanikisha kwa kiasi kikubwa na kuongeza kuwa, wameboresha tofauti na miaka mingine iliyopita.

Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Ombeni Zavalla, alisema wamekubaliana na waandaaji wa mashindano hayo kwa sababu wana vigezo vyote vya kuandaa ikiwemo kibali kutoka shirikisho hilo.

Alisema mbio hizo zimekuwa mfano kwa waandaaji wengine kutokana na kuwa imekuwa ikilipa zawadi kwa wanariadha kulingana na zile walizotangaza.

"Cha msingi zawadi katika mashindano haya lazima ziwepo, ili kuepusha migogoro na malumbano ambayo huwa yanajitokeza mara kwa mara endapo waandaaji wanaposhindwa kutoa zawadi walizoahidi kwa washiriki,” alisema Zavalla.

Alisema kutokana na hilo, wanapaswa kuandaa askari ambao watasaidia katika suala zima la ulinzi wakati mashindano hayo yakiendelea.

Kwa upande wa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Ayoub Magimba, alisema michezo inasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza magonjwa ambayo yanaonekana sugu kwa jamii isiyokuwa na mazoezi.

No comments:

Post a Comment

Pages