Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Dar es Salaam (DRFA) kimesitushwa na kufadhaishwa na maamuzi yaliyofanywa na
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kutangazwa kwenye vyombo mbali
mbali vya habari bila ya kufuata misingi ya KATIBA na KANUNI zinazoongoza
katika usimamizi wa mpira katika nchi yetu.
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Dar es Salaam baada ya kupitia KATIBA na KANUNI za TFF, DRFA, na KIFA
kimejiridhisha kwamba maamuzi yaliyofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) ya kufuta matokeo halali ya uchaguzi wa Chama Cha Mpira wa Miguu
Wilaya ya Kinondoni uliofanyika siku ya Jumapili tarehe 12/06/2016 katika bwalo
la maofisa wa polisi Oysterbay bila hayakuzingatia KATIBA na KANUNI za TFF,
DRFA na KIFA.
Maamuzi hayo ya TFF yamevunja
katiba ya TFF, DRFA na KIFA pamoja na kanuni zake ambazo ndiyo mwongozo wa
mpira wetu hasa katika upatikanaji wa mamlaka za uendeshaji wa mpira katika
ngazi mbalimbali za taifa, mkoa na wilaya.
Katiba ya TFF ibara ya 52(2) na ibara ya 52(6)(a)
zinaeleza wazi kazi na majukumu ya kamati ya uchaguzi ya TFF ni kwa chaguzi za
TFF na wanachama wake ambao ni vyama vya mikoa, vilabu vya ligi kuu na
kusimamia uchaguzi wa Board ya ligi pamoja na kuishauri kamati ya utendaji
mambo yanayo husiana na chaguzi hizo.
Kwa mujibu wa katiba ya TFF ya
2013 kamati yake ya uchaguzi haiwajibiki na lolote kwa vyama vya mpira wa miguu
vya wilaya ambao si wanachama wa TFF. Lakini pia Ibara ya 3(i) ya kanuni za uchaguzi za TFF za 2013 inaeleza kuwa
kamati ya uchaguzi ya TFF itaendesha na kusimamia uchaguzi wa TFF na Bodi ya
Ligi.
Ibara
ya 6 ya kanuni za uchaguzi za TFF za 2013 pia inaeleza majukumu ya kamati ya uchaguzi na katika
majukumu yake hakuna popote inapoonyesha kuwa ina mamlaka ya kusimamia na
kutolea maamuzi chaguzi za vyama vya mpira wa miguu vya wilaya ambao si
wanachama wa TFF.
Kwa mujibu wa Katiba ya KIFA ibara ya 47 na kanuni za
uchaguzi kipengele (b) inasema Kamati ya Uchaguzi ya KIFA itafanya kazi kwa
kushirikiana na sekretarieti ya Chama na chini ya uangalizi na Miongozo ya
Kamati ya Uchaguzi ya DRFA. Kwahiyo ni jukumu la kamati ya uchaguzi ya DRFA
kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kugundua kwamba Kamati yake ya Uchaguzi
haina mamlaka ya KIKATIBA kuweza kusimamia chaguzi za vyama vya wilaya,
miongoni mwa mapendekezo ya mabadiliko ya KATIBA waliyoleta katika Mkutano Mkuu
wa TFF wa mwisho uliofanyika Tanga ni pamoja na hilo kuuomba MKUTANO MKUU wa
TFF uweze kufanya hilo badiliko ili waweze kusimamia chaguzi za WILAYA lakini
BAHATI mbaya marekebisho ya KATIBA hayakuweza kupitishwa na wajumbe wa MKUTANO
Mkuu.
Katiba ya KIFA katika kanuni zake za uchaguzi 5 (h) inatamka
kwamba RUFAA zote zihusuzo uchaguzi zitawasilishwa kwenye kamati ya RUFAA ya
Wilaya na hatimae kama Mrufani hakuridhika basi atakata RUFAA katika kamati ya
RUFAA ya Mkoa ambapo uamuzi wake utakuwa ndio wa MWISHO.
Baada ya Mwenyekiti wa Kamati
ya Uchaguzi ya KIFA kutangaza matokeo ya uchaguzi huo tajwa hapo juu na
kutuletea ripoti yake, mmoja wa wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti Bwana Thomas
Mazanda aliamua kukata RUFAA katika Kamati ya uchaguzi ya Chama Cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kama katiba ya KIFA inavyoelekeza KUPINGA
matokeo yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi wa KIFA. Lakini cha kushangaza wakati kamati ya
uchaguzi ya DRFA ikipanga kusikiliza RUFAA hiyo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) likaitisha kikao 18/06/2016 na kuamua KUFUTA uchaguzi huo bila kufuata
taratibu za KIKATIBA na KIKANUNI zinazotuongoza.
Kamati ya Uchaguzi ya Chama Cha
Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni kwa mujibu wa Ibara ya 47 inaundwa na wajumbe watano. Wajumbe wa kamati hii
watateuliwa na Mwenyekiti. Na Mwenyekiti wa kamati hii lazima awe ni
mwanasheria na wajumbe wengine wane lazima wawe ni watu wenye ujuzi na upeo
katika masuala ya michezo. Kwa mujibu wa katiba ya KIFA haina makamu mwenyekiti
wala katibu wa kamati. Na maadam KATIBA inatamka wazi Mwenyekiti lazima awe
mwanasheria TAFSIRI yake ni kwamba bila uwepo wa Mwenyekiti kamati haiwezi
kuendelea na kazi zake kwa sababu ukiondoa Mwenyekiti wajumbe wengine waliobaki
wa kamati ya KIFA hawana taaluma ya SHERIA.
Katika kuakikisha uchaguzi huo
wa KIFA una kuwa huru na haki Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya KIFA alialika watu tofauti tofauti kuhudhuriailia
katika uchaguzi huo wakiwemo mwakilishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Mwenyekiti wa SPUTANZA Taifa na Mjumbe Mmoja wa Kamati ya Utendaji ya
TFF katika uchaguzi huo.
Kwa mlolongo huu wa matukio ni
dhahiri TFF imepora mamlaka ya kamati ya uchaguzi ya KIFA na DRFA kwa kuingilia
na kufuta uchaguzi wa KIFA ambaye KIKATIBA ni mwanachama wa DRFA. Lakini pia
TFF hii imefanya MAAMUZI yanayofanana na hayo katika uchaguzi wa Chama Cha
Mpira Miguu Wilaya ya Temeke.
Uporaji huu wa madaraka ya
mwanachama wa TFF ni HATARI, BATILI
na KINYUME cha utaratibu tuliojiwekea
hivyo kufanya hata MAAMUZI hayo yaliyofanywa na TFF kuwa BATILI. Hii inatokana
na ukweli kuwa kutokana na katiba zetu TFF haina nguvu yoyote ya kikatiba wala
kikanuni ya kutolea maamuzi mchakato wa uchaguzi wa chama cha wilaya ambaye ni
mwanachama wa chama cha mpira wa miguu cha mkoa.
kwa haya yanayoendelea katika
TFF ni dhahiri kuwa taasisi hiyo sasa inaondokana na utaratibu wa kuendesha
mambo yake kwa kuegemea misingi ya KATIBA na KANUNI zake na badala yake kuendesha
mambo yake ki – imla. Ni jambo la hatari kwa taasisi kubwa kama TFF kuendesha
mambo yake ki – imla kwani itapoteza heshima iliyojijengea kwa miaka mingi.
Ni matumaini yetu kuwa HAKI
itasimamiwa ipasavyo
Imetolewa na
Chama
Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment