HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 29, 2016

MPOTO AHIMIZA VITA YA UKIMWI

Balozi wa Kili Challenge ambaye pia ni msanii wa muziki wa kughani, Mrisho Mpoto akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, kuhusu tukio la kupandisha watu 50 katika kilele cha mlima Kilimanjaro na waendesha baiskeli 50 watakaozunguka mlima huo kwa baiskeli ili kuchangisha fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya Ukimwi. Kulia ni Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), Tenga Tenga. na kushoto ni Kamishina wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Peter Dickson.
Balozi wa Kili Challenge ambaye pia ni msanii wa muziki wa kughani, Mrisho Mpoto akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu tukio la kupandisha watu 50 katika kilele cha mlima Kilimanjaro na waendesha baiskeli 50 kuuzunguka mlima huo kwa baiskeli ili kuchangisha fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya Ukimwi. Kulia ni Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), Tenga Tenga. (Picha na Francis Dande)    

NA FRANCIS DANDE

MGODI wa Dhahabu wa Mkoani Geita ambao umekuwa ukishirikiana na Tume ya Kudhibiti Ukimwi tangu kuanzishwa kwake miaka 15 iliyopita, unataraji kupandisha watu 50 katika kilele cha mlima Kilimanjaro maarufu kama ‘Kili Challenge’ ili kuchangisha fedha za mapambano dhidi ya Ukimwi.

Mbali ya idadi hiyo kupanda kileleni mwa mlima huo mrefu zaidi barani Afrika, kutakuwa na waendesha baiskeli 50 ambao watazunguka mlima huo kwa baiskeli, yote hiyo katika kampeni hiyo ya kusaka fedha
za kusaidia mapambano ya ugonjwa wa Ukimwi.

Meneja wa Mawasiliano na Mahusiano  wa Mgodi wa GGM, Tenga Tenga, alisema jana kwamba, tukio hilo limalovuta hisia za wengi kutoka ndani na nje ya Tanzania wakiwamo wanaharakati wa vita dhidi ya ukimwi, litafanyika kuanzia Julai 16 hadi Agosti 22.

“Kilimanjaro Challenge kwa mwaka huu itakuwa na kundi kubwa la watu kutoka ndani na nje ya Tanzania, japo wengi wao watakuwa kutoka hapa nchini wakiwamo kutoka sekta binafsi, serikalini, wawakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN)  waliojitolea kuchangia mfuko huo wa Kili Challenge. Balozi wetu Mpoto ndiye ataambatana na kundi hili hadi kileleni,” alisema Tenga.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mpoto amewasihi watanzania kutambua mapambano dhidi ya Ukimwi ni jukumu la wote, hivyo ni jukumu la wote ili kufikia dhamira ya sifuri tatu kwa maana ya kumaliza kabisa maambukizi mapya, unyanyapaa pamoja na vifo.

“Mimi kama Balozi wa Kili Challenge  naamini jitihada zinazofanywa na  mfuko huu zinahitaji kuungwa mkono na watanzania wote na wadau wenye machungu na nchi hii. Hebu  tuungane kwa pamoja, kila mmoja kwa sehemu yake, iwe kwa kuchangia ama kuelimisha mwingine ili mapmbano haya yalete manadiliko,” alisema Mpoto.

Naye Mwakilishi wa Tacaids, Dickson Peter, alisema fedha zitakazopatikana zitapelekwa kusaidia mapambano dhidi ya ukimwi ikiwemo kujenga  vituo vya ushauri nasaha na upimaji wa ukimwi ambapo baadhi yao ni vile vilivyopo Segera Mkoani Tanga, Manyoni na Geita.

Peter aliyataja matunda mengine ya Kili Challenge, ni kituo cha watoto Yatima Moyo wa Huruma na asasi nyingine zaidi ya 30 ambazo tayari zimenufaika na mfuko huu tangu uanzishwe na kusema GGM, inatambua  pia sapoti ya wadau wengine kama Acacia, Prime Fuel, Artel, Capital Drilling (T) Ltd na wengineo.

No comments:

Post a Comment

Pages