HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 28, 2016

SERENGETI BOYS YATUA SALAMA MADAGASCAR

Msafara wa timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, uliondoka jana alfajiri Dar es Salaam, Tanzania imetua salama jijini Antananarivo, Madagascar kwa ajili kambi ya siku 10 kujiandaa na mchezo dhidi ya Afrika Kusini kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika utakaofanyika Agosti 6, 2016.

Mchezo wa marudiano utafanyika Agosti 21, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam, ulioko Chamazi-Mbagala, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam na kwamba mshindi atakuwa amejiwekea mazingira mazuri ya kuwania nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana, zitakazofanyika mwakani huko Madagascar.

Mkuu wa msafara akiwa ni Ayoub Shaibu Nyenzi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Soka la Vijana, maofisa wengine waliosafiri na timu hiyo ni Kocha Mkuu, Bakari Nyundo Shime maarufu zaidi kwa jina la Mchawi Mweusi, Daktari wa timu hiyo, Shecky Francis Mngazija na Mtunza Vifaa, Andrew Vanance Andrew.

Pia yumo Juma Kaseja Juma ambaye kwa muda amechukua nafasi ya makocha wasaidizi, Sebastian Nkoma na Muharam Mohammed ‘Shilton’ wanaohudhuria kozi ya makocha ngazi ya juu inayoratibiwa na CAF.

Nyota waliosafiri ni pamoja na makipa, Ramadhani Awm Kabwili, Kelvin Deogratius Kayego na Samwel Edward Brazio wakati mabeki wako Kibwana Ally Shomari, Nickson Clement Kibabage, Israel Patrick Mwenda, Dickson Nickson Job, Ally Hussein Msengi, Issa Abdi Makamba na Enrick Vitalis Nkosi.

Viungo ni Kelvin Nashon Naftal, Ally Hamisi Ng’anzi, Asadi Ali Juma Ali, Syprian Benedictor Mtesigwa, Ibrahim Abdallah Ali, Shaban Zuberi Ada huku washambuliaji wakiwa ni Mohammed Abdallah Rashid, Yohana Oscar Mkomola na Muhsin Malima Makame.

Serengeti Boys inakwenda kucheza na Afrika Kusini baada ya kuwatoa Shelisheli kwa jumla ya mabao 9-0 katika mechi zake mbili za kimataifa. Mshindi wa jumla kati ya Serengeti Boys na Afrika Kusini, atacheza na timu mshindi kati ya Namibia na Congo-Brazaville.

Hivi karibuni Serengeti Boys ilifanya ziara India ambako walishiriki mashindano ya vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International Youth Tournament 2016) kabla ya kurudi na rekodi ya kupigiwa mfano si tu katika Tanzania na kwa nchi za Afrika Mashariki. Ilishika nafasi ya tutu nyuma ya Korea Kusini na Marekani.#

No comments:

Post a Comment

Pages