HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 25, 2016

MAJALIWA: TATIZO LA MAJI SUMBAWANGA KUWA HISTORIA


 2814 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakiwapungia wananchi wa Kijiji cha Mtowisa  baada ya kuwasili kijijini hapo wakiwa katika ziara ya mkoa wa Rukwa Agosti 24, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Wananchi wa kijiji cha Mtowisa mkoani Rukwa wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia mkutano wa hadhara kijijini hapo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakifurahia ngoma ya asili ya kabila la Wafipa wakati walipowasili kwenye kijiji cha Mtowisa mkoani Rukwa kuzungumza na wananchi.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary  wakiwapungia wananchi wa kijiji cha Mtowisa baada ya kuwasili kwenye kijiji cha Mtowisa mkoani Rukwa

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa inatarajiwa kupata huduma ya maji safi na salama kuanzia mwezi ujao baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji uliokuwa unajengwa.
 
Mradi huo unajengwa kwa usimamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, Manispaa ya Sumbawanga (SUWASA), kwa ufadhili wa nchi za Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya Ujerumani kupitia benki yake ya Maendeleo (KfW), sh. bilioni 31 utakapokamilika.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana  (Jumatano, Agosti 24, 2016) wakati na akiweka jiwe la msingi la mradi wa maji safi na usafi wa mazingira katika Manispaa ya Sumbawanga na kuitaka kampuni ya kampuni ya Techno Fab Gammon Joint Venture ya India kumaliza ujenzi wa mradi huo haraka iwezekanavyo.

Alisema mradi huo ambao tayari umekamilika kwa asilimia 85 unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu, hivyo aliwataka wananchi kuhakikisha wanashirikiana na Manispaa katika kulinda miundombinu ya mradi huo mara utakapokamilika pamoja na kutunza vyanzo vya maji.

“Pamoja na Serikali kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kugharamia miradi ya maji inayojengwa katika maeneo mbalimbali nchini,changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo imekuwa kubwa kutokana na baadhi ya visima vimeanza kukauka hali inayosababishwa na uharibifu wa mazingira,” alisema.

Alisema kumekuwa na uvamizi mkubwa katika maeneo ya vyanzo vya maji ambapo wananchi wanajishughulisha na shughuli za ulimaji, uchungaji wa mifugo, ujenzi wa nyumba za makazi na uchomaji misitu hivyo kusababisha uchafuzi wa mazingira na hatimaye vyanzo hivyo hukauka.

Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu amewaagiza wakuu wote wa wilaya na wenyeviti wa vijiji nchini kuyasimamia maeneo yenye vyanzo vya maji na kuwaondoa watu wotewalioyavamia kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria pamoja na kuwafikisha mahakamani.

Naye Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe ambaye alimuwakilisha Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge katika hafla hiyo alisema aliishukuru Serikali ya Ujerumani na Umoja wa nchi za Ulaya kwa kufadhili mradi huo.

Hata hivyo Mhandisi Kamwelwe alisema suala la kuhifadhi mazingira ni msingi endelevu wa upatikanaji wa maji safi na salama, hivyo aliwaomba wananchi kujiepusha na uchafuzi wa vyanzo vya maji na uharibifu wa mazingira ili kuepuka athari ya Taifa kukubwa na janga la ukame.

“Wananchi wanatakiwa kuacha kufanya shughuli za maendeleo ikiwemo kulima, kufuga ndani ya mita 60 kutoka katika mito, maziwa na vyanzo vingine vya maji ili kuepusha uharibifu wa mazingira ambao madhara yake ni makubwa kwa viumbe wote,” alisema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMIS, AGOSTI 25, 2016.

No comments:

Post a Comment

Pages