HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 22, 2016

Tume ya Mipango yaendesha Warsha kujenga uelewa juu ya Mipango ya Maendeleo ya Kimataifa na Kikanda


Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Balozi Innocent Shiyo (katikati) kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa akitoa hotuba ya ufunguzi wa warsha ya kufungamanisha sera, mikakati na mipango ya maendeleo ya kitaifa na ile ya kimataifa na kikanda iliyofanyika Septemba 22, 2016 katika ukumbi wa  kituo cha mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anayesimamia Klasta ya Biashara za Kimataifa na Mahusiano ya Uchumi, Bw. Paul Sangawe na kulia ni Bw. Maxwell Mkumba kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).


Na Adili Mhina


Tume ya Mipango kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa pamoja na Sekretarieti ya Jumuiya ya Nchi za kusini mwa Afrika (SADC) imeendesha warsha ya kujenga uelewa juu ya Dira na mipango ya maendeleo ya  kimataifa na kikanda.

Warsha hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa kituo cha  mikutano cha Mwalim Julius Nyerere, Dar es salaam imewakutanaisha wakurugenzi wa mipango na sera kutoka sekta mbalimbali, idara na mashirika ya Umma, wawakilishi wa asasi zisizo za kiraia, wawakilishi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali pamoja na wataalam kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Akifungua warsha hiyo Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Innocent Shiyo alieleza kuwa Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza makubaliano mbalimbali kikanda na kimataifa kwa lengo la kutumia fursa zinazopatikana kwa nchi wanachama ili kuongeza kasi ya maendeleo.

Balozi Shiyo alieleza kuwa ni muhimu wadau wanaohusika na masuala ya sera na mipango nchini kuwa na uelewa wa kutosha juu ya namna sera, mikakati na mipango ya maendeleo ya kimataifa na kikanda iliyofungamanishwa na ile ya kitaifa ili kuhakikisha utekelezaji wake unaenda sambamba.

“Tanzania ni mwanachama wa umoja wa mataifa na ipo mstari wa mbele katika kutekeleza makubaliano mbalimbali ikiwemo agenda ya maendeleo endelevu 2030, programu ya kutekeleza makubaliano ya Instanbuli (2010-2020), nk. Vile vile ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika, nk. Hivyo, ni muhimu kujua malengo ya jumuiya hizi na kuangalia namna mipango yetu ya ndani inavyotusaidia kufikia malengo ya nje”, alisema.

Naye Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anayesimamia Klasta ya Biashara za Kimataifa na Mahusiano ya Uchumi, Paul Sangawe alisema kuwa warsha hiyo itasaidia kujenga uelewa juu ya Sera, mikakati na mipango ya maendeleo ya kimataifa na kikanda hususani malengo ya maendeleo endelevu 2030, Agenda ya maendeleo ya Afrika 2063, na mpango mkakati wa nchi za kusini mwa Afrika 2016/17-2010/21.

Aliongeza kuwa warsha hiyo itasaidia kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa sera, mikakati na mipango ya maendeleo ya kimataifa na kikanda.

Vile vile warsha hiyo itasaidia kutoa uzoefu kutoka nchi zingine ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

No comments:

Post a Comment

Pages