HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 30, 2016

WAZIRI MKUU APOKEA MICHANGO YA SH. MILIONI 190

 Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akipokea hundi ya shilingi  milioni 220.


xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea jumla ya sh. milioni 190 kutoka kwa balozi wa Pakistan nchini Mhe. Amir Khan, Kaimu Balozi wa China Mhe. Gou Haodong na Taasisi ya Aga Khan.

Fedha hizo zimetolewa ili kusaidiia  wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 walijeruhiwa.

Pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.

Makabidhiano ya michango hiyo, yamefanyika leo (Ijumaa, Septemba 30, 2016) kwenye Hotel yaHyatt Regency jijini Dar Es Salaam ambapo Waziri Mkuu aliwashukuru kwa michango hiyo na alitumia fursa hiyo kuwaomba wale walioahidi kutoa michango wakamilishe ahadi zao.

“Ninawaomba wale walioahidi kutoa michango wakamilishe ahadi kwa kuzileta ofisini kwangu au kutuma kupitia akaunti ya maafa iliyofunguliwa katika Benki ya CRDB yenye Namba. 015 222 561 7300 kwa jina la KAMATI MAAFA KAGERA – Swiftcode: CORUtztz,” amesema.

Amesema watu walio mbali na benki watumie namba za simu zilizotolewa mahsusi kwa ajili ya kupokea michango ya maafa hayo ambazo ni 0768-196-669 (M-Pesa), au 0682-950-009 (Airtel Money) au 0718-069-616 (Tigo Pesa).

Akikabidhi hundi kwa Waziri Mkuu, Balozi wa Pakistan, Mhe. Amir alisema wanaamini mchango huo wa sh. milioni 80 walioutoa utasaidia kuwapunguzia uchungu wananchi wa Kagera kutokana na athari zilizosababishwa na tetemeko la ardhi.

Kwa upande wake Kaimu Balozi wa China Mhe. Haodong alimweleza Waziri Mkuu kwamba wameshtushwa na tukio hilo na tayari walishawapeleka madaktari na wataalamu wengine mkoani Kagera na leo walikuwa wanakamilisha ahadi yao ya kutoa mchango wa sh. milioni 60.
Naye Muwakilishi Mkazi wa Taasisi za Aga Khan nchini, Amin Kurji  alimkabidhi Waziri Mkuu hundi ya sh. milioni 50.
                               
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
IJUMAA, SEPTEMBA  30, 2016 

No comments:

Post a Comment

Pages