HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 10, 2016

MFUMUKO WA BEI WAPUNGUA

Na Mwandishi Wetu

MFUMUKO wa bei wa Taifa kwa Septemba mwaka huu umepungua hadi asilimia 4.5 kutoka asilimia 4.9  kwa Agosti mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Albina Chuwa, alisema hiyo haimaanishi kuwa vitu vimepungua bali kilichopungua ni kasi ya kupungua kwa bei.

Alisema fahirisi za bei zimeongezeka hadi 103.05  Septemba  2016 kutoka 98.64 ya Septemba mwaka jana na kuongeza kuwa mfumuko wa bei kwa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi Septemba mwaka huu umepungua hadi asilimia 6.0 kutoka asilimia 7.0 ya Agosti mwaka huu.

“Kupungua kwa mfumuko wa bei Septemba mwaka huu kumechangiwa na kupungua kwa bei ya baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia Septemba 2016 zikilinganishwa na bei za Septemba 2015”alisema Chuwa.

Alisema mwenendo wa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonesha kupungua ni pamoja na bei za Dagaa kwa asilimia 11.6 na Viazi vitamu kwa asilimia 3.2.

Aliongeza kuwa kwa upande mwingine mwenendo wa bei za baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zillionesha kupungua ni pamoja na bei za Gesi kwa asilimia 10.4, Dizeli kwa asilimia 2.9 na Petroli kwa asilimia 2.8.

Alisema mabadiliko ya bei kati ya Agosti na Septemba mwaka huu fahirisi za bei zimepungua hadi 103.05 Septemba mwaka huu kutoka 103.28 Agosti mwaka huu.

“Kupungua kwa fahirisi za bei kumechangiwa na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula” alisema Chuwa.
Alitaja baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa fahirisi kuwa ni pamoja na Mchele kwa asilimia 2.6, unga wa mahindi kwa asilimia 1.0, Dagaa asilimia 3.0 na mbogamboga kwa asilimia 4.3.

Alisema kwa upande mwingine kwa baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei ni pamoja na Dizeli kwa asilimia 2.9, Petroli asilimia 2.8 na mafuta ya taa kwa asilimia 2.9.

Aidha alisema uwezo wa Sh. 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umefikia Sh.97 na Senti 04 Septemba 2016 kutoka Desemba, 2015 ikilinganishwa na Sh.96 na Senti 83 ilivyokuwa Agosti mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Pages