HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 28, 2016

WAZIRI MKUU ACHANGIA MABATI UJENZI WA ZAHANATI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewahimiza wakazi wa vijiji saba wilayani Ruangwa waharakishe kufyatua matofali ili waanze ujenzi wa zahanati na yeye atawachangia mabati.

Ametoa ahadi hizo leo (Jumatano, Desemba 28, 2016) wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Namilema, Mbuyuni, Nandandara, Namkonjera, Muhuru, Chikundi na Chibula na viongozi wa wilaya ya Ruangwa, mkoa wa Lindi ambako anapita kuwasalimia wananchi wa jimbo lake na kuhimiza kazi za maendeleo. Waziri Mkuu yuko Ruangwa kwa siku nne kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.

Amesema sera ya Serikali ni kuwa na zahanati kwa kila kijiji na kituo cha afya kwa kila kata na kwamba umefika wakati wa kuanza kutekeleza kaulimbiu ya jimbo hilo inayosema “Ruangwa kwa maendeleo, inawezekana.”

Katika kuhimiza ujenzi wa zahanati hizo, amechangia mabati kati ya 50 na 150 kwa kila kijiji na akawahimiza wahakikishe wanakamilisha mapema ujenzi wa maboma ili aweze kutimiza ahadi yake ya mabati.

Amesema katika awamu iliyopita, alikazania sana suala la elimu kwa kusimamia ujenzi wa nyumba za walimu na madarasa kwenye shule ambazo hazikuwa na madarasa ya kutosha. Pia alisimamia ukarabati wa majengo chakavu katika baadhi ya shule.

“Kuanzia awamu hii na miaka minne iliyobakia, mkakati wangu ni kusimamia upatikanaji wa maji safi na suala la kuboresha sekta ya afya katika jimbo zima nikishirikiana na uongozi wa Halmashauri yetu,” amesema.

Pia amemwagiza Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Japhet Simeo ahakikishe anawasiliana na viongozi wa vijiji hivyo ili wapatiwe michoro ya ramani zilizoidhinishwa na Wizara ya Afya.

Wakati huohuo, Mkurugenzi wa kampuni ya Umemejua ya Baraka Solar Specialist, Bw. Ansi Mmasi amesema atajitolea kuweka mfumo wa umemejua wa watts 300 pamoja na nyaya zake kwenye zahanati inayotaka kujengwa kwenye kijiji cha Namilema.

Alisema anaishukuru kwa kuwapa kazi makandarasi wazawa na akawataka wakandarasi wenzake watumie vifaa bora na imara pindi wanapopewa kazi ya kutoa huduma na taasisi mbalimbali ikiwemo halmashauri na idara za Serikali.

“Tujitahidi kufanya kazi hizi kwa weledi na tutumie vifaa bora na imara ili watu wanaotarajia huduma zetu waweze kuridhika na kuendelea kuwa na umani na wakandarasi wazawa kwamba tunaweza kufanya kazi nzuri na zenye ubora unaotakiwa,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Wanyumbani Construction, Bw. Fakihi J. Bakili alisema atachangia mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo ya kijiji cha Namilema. Pia alichangia mifuko 100 kwenye zahanati ya kijiji cha Manokwe na mifuko mingine 50 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Chikundi.

                            
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, DESEMBA 28, 2016.

No comments:

Post a Comment

Pages