HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 28, 2016

ZANTEL YAILIPA MANISPAA YA KINONDONI MILIONI 687

MKUU wa Wilaya ya Kinondoni Ally Hapi amesema Kampuni ya Simu za mikononi ya Zantel imelipa kiasi cha zaidi ya Sh. Milioni 687 ilichokuwa inadaiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Kampuni ya Zantel ilikuwa inadaiwa kiasi hicho cha fedha ambazo zinatokana na kuingia mkataba tangu mwaka 2009 wa eneo walilolipangisha kutoka katika halmashauri hiyo.

Kutokana na kutolipa deni hilo kwa muda wa miaka nane tangu kusainiwa kwa mkataba mkuu huyo wa wilaya alitoa siku saba kwa kampuni hiyo kuhakikisha wanalipa kiasi hicho cha fedha wanachodaiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Hapi alisema fedha walizotoa Zantel zote zinaelekezwa katika kujenga vyumba vya madarasa 40 katika wilaya hiyo.

Alisema manispaa hiyo inaupungufu wa vyumba vya madarasa 79 kiasi kinachosababisha  wanafunzi 3169 waliofaulu kushindwa kuendelea na masomo hivyo fedha hizo zitajenga madarasa ili kupunguza tatizo hilo.

“Kwanza naipongeza kampuni ya Zantel kwa kutii agizo letu tulilowapa kwani wameweza kutulipa fedha zote tulizokuwa tunawadai, kutokana na kuwapo kwa tatizo la upungufu wa madarasa katika manispaa yetu fedha zote zilizolipwa kiasi cha Sh. Milioni 687 zinaelekezwa katika kujenga madarasa 40 kati ya 79 tunayoyahitaji.

“Hata hivyo nimeshamuagiza Mkurugenzi kutafuta eneo la wazi ili tuweze kuangalia kama tutaweza kujenga shule moja kupitia fedha hizi na tayari nimeshapata taarifa kuwa kuna eneo la wazi huko Salasala ambalo limetolewa na wananchi kwaajili ya kujenga shule na wanahitaji sapoti  kutoka serikalini  ,” alisema.

Hapi alisema pamoja na Zantel kulipa deni hilo lakini bado vyombo vya dola vinaendelea na kazi yake ya uchunguzi wa kubaini ni kwanini fedha hizo hazikulipwa kwa muda wote na kina nani wanahusika katika sakata la kufisha mkataba waliosaini na manispaa hiyo.

“Vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi ili kubaini wale waliokuwa wameufisha mkataba huo na ni kwanini fedha hizo zimechukua muda mrefu bila kulipwa, watakapomaliza watatuambia na sisi tutachukua jukumu la kuwaeleza wananchi hivyo nawaomba watu wasiwe na wasiwasi,” alisema.

Hata hivyo Hapi amewaagiza wakurugenzi wote katika mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha wanajipanga vizuri katika kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa yanayotaka kila wanafunzi aliyefaulu anakwenda shule ya sekondari na si kukaa nyumbani.

Aidha Hapi ametoa wito kwa makampuni yanayodaiwa na manispaa hiyo kuanza kujisarimisha mapema kwa sababu sasa hivi wameanza kufanya oparesheni ya kubaini mikataba iliyoingiwa na hafatiliwi lengo likiwa kuhakikisha mapato ya serikali yanapatikana.

No comments:

Post a Comment

Pages