HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 04, 2017

ACT WAZALENDO: UGUMU WA KUTATUA CHANGAMOTO ZA MAENDELEO ZINASABABISHWA NA OMBWE LA UONGOZI

NA SAIDI POWA, SONGEA

ALIYEKUWA Mgombea wa Urais wa Chama cha ACT Wazalendo na Mwenyekiti wa Chama hicho, Anna Mghwira, amesema kumekuwa na ombwe la uongozi ndani ya nchi kwa muda mrefu.

Hali hiyo imekuwa ikiongeza ugumu wa kutatua changamoto za maendeleo ndani ya nchi na kusababisha wananchi kupata shida kila siku.

Mghwira aliyasema hayo wakati akiwahutubia wanachi wa Kata ya Tanga Manispaa ya Songea, katika mkutano wa kampeni za udiwani za kata hiyo mjini hapa jana.

Aidha alifafanua kuwa matatizo yanayowakuta wananchi wa maeneo mbalimbali ikiwemo kata hiyo yanatokana na kutokuwepo kwa uongozi unaowajibika kwa wananchi na kuto onyesha ushirikiano katika kuleta maendeleo.

Mwenyekiti huyo alishangazwa na taarifa za kucheleweshwa kwa pembejeo za kilimo, wakati huu wakulima wakiwa wanapalilia mahindi yao, lakini ndio pembejeo za ruzuku zinaletwa bila ya kueleza sababu za kuchelewa kwake.

Mkoa wa Ruvuma ni mkoa unao ongoza kwa uzalishaji wa zao la mahindi nchini lakini kutokana na ucheleweshwaji huo wa pembejeo unaweza kuathiri uzalishaji wa zao hilo.

Kwa kawaida pembejeo hizo zinatakiwa kusambazwa kwa wakulima mwezi wa 10, ili zianze kupandwa mwezi wa 11 na 12, lakini wakulima wengi ambao walikosa pembejeo hizo mwaka jana ndio wanaanza kupanda sasa.

Akisisitiza kuwepo kwa ombwe la uongozi katika serikali alisema kitendo cha kushindwa kujenga vivuko (madaraja) katika mito mingi iliyopo mkoani humo ni aibu kwa sababu serikali inajua vizuri jiografia ya mkoa huo.

"Hivi vidaraja vidogovidogo havi hitaji pesa nyingi, kinachotakiwa ni ushirikiano kati ya viongozi na wananchi na kuweza kuvijenga lakini kwakuwa viongozi wako mbali na wananchi ndio maana kuna matatizo ambayo hayana sababu ya kuwepo," alisema.

Kutokuwepo kwa madaraja kumekuwa kukisababisha vifo vya watu hasa wanafunzi wakati wa masika wanapojaribu kuvuka mito hiyo wakienda au wakirudi shuleni.

Nae mgombea wa udiwani katika kata hiyo ya Tanga, Engerebeth Mponda 'Swahiba' aliwaambia wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa pamoja na kero nyingi zilizopo kwenye kata hiyo lakini tatizo la shule kuwa ziko mbalimbali atalitatua kwa kuanzisha ujenzi wa shule nyingine.

"Katika elimu tuna changamoto ya hizi shule zetu, ziko mbalimbali mno, hivyo kuna kila sababu ya kujengwa shule nyingine hapa katikati, ili kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu watoto wetu," alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages