HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 10, 2017

Mromania Kocha Mpya Azam FC

Kocha Mkuu wa Azam FC,  Aristica Cioaba, akisaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo leo.

Dar es Salaam, Tanzania

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, mchana huu imemtangaza, Aristica Cioaba, kuwa Kocha Mkuu wa kikosi hicho.
Cioaba, 45, anakuja Azam FC kurithi mikoba ya Mhispania Zeben Hernandez, aliyesitishiwa mkataba pamoja na benchi lake zima la ufundi.
Kocha huyo atasaidiana na makocha wazawa, Idd Nassor Cheche na Kocha wa Makipa Idd Abubakar, walioiongoza timu hiyo kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambapo saa 10.15 jioni ya leo itasaka fainali kwa kukipiga na Taifa ya Jang’ombe.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Ofisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Saad Kawemba, tayari wamefanikiwa kumpata kocha huyo na wameingia naye mkataba wa muda wa miezi sita wenye kipengele cha kuongezwa.
Alisema Cioaba ana uzoefu mkubwa wa soka la Afrika na ataiongoza Azam FC kwa kipindi hiki hadi mwishoni mwa mwa msimu, ambapo baada ya kuisha watakaa tena mezani kufanya tathimini ya mafanikio yake na wapi wanaweza kuendelea kutokana na kazi iliyofanyika.
“Bodi ya Wakurugenzi ya Azam FC inapenda wadau wote wa mpira na wapenzi na mashabiki wa Azam kwamba klabu imempata mwalimu, ambaye ndiye ataiongoza klabu kwa kipindi hiki hadi mwishoni mwa msimu.
“Kwa hiyo kwa mashabiki wetu maana yake ni kwamba tukiingia kwenye mechi inayofuata ya ligi, kocha atakuwa ameanza kazi na Cheche (Idd Nassor) atakuwa msaidizi wake na benchi lake zima alilokuwa nalo hivi sasa litaendelea,” alisema.
Kawemba aliongeza kuwa hivi sasa kocha huyo atakuwa na kikosi visiwani Zanzibar kufuatilia mwenendo wa timu ulivyo na ataendelea kutoa ushauri panapohitajika na ataanza rasmi kukaa kwenye benchi mpaka pale vibali vyake vya kufanya kazi nchini vitakapokamilika.
“Taratibu hizo zitakwenda kwa mujibu wa sheria za nchi, ambapo tutaziheshimu na kuona ya kwamba tutazifanya kwa haraka zaidi ili mwalimu aweze kupata kibali cha kufanya kazi hapa nchini, kwa hayo machache tunawaomba mashabiki wetu wawe watulivu wampe sapoti kocha na wadau wote wa mpira waone ya kwamba tumefanya jambo la kheri,” alisema.
Kauli ya kwanza ya Cioaba
Kwa upande wake Cioaba, alisema kuwa anafuraha kubwa leo hii kusaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo huku akiahidi kazi nzuri na kuifanya timu hiyo kuwa bora.
“Najua Azam FC hapa Tanzania ni moja ya timu kubwa yenye historia huko nyuma, napenda kuushukuru uongozi kwa kuniamini na kunipa nafasi kuja kufundisha soka kwenye nchi hii, kwa mashabiki napenda kuwaambia kuwa nalijua soka la Afrika, nimewahi kufundisha Ghana na kupata matokeo mazuri.
“Kuhusu wakati ujao, nina furaha sana kuhusu uongozi walipoongea na mimi wakati tunaweka mipango ya timu ya hapo baadaye na hili ni jambo zuri kwa kocha, kitaaluma nawaahidi mashabiki na watu wote wanaoipenda Azam FC, niko hapa kuwapa mambo mazuri katika kazi yangu kwenye klabu,” alisema.
Msimu uliopita, Cioaba aliiongoza Aduana Stars ya Ghana kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Ghana, ambapo anafahamiana kwa ukaribu na nyota wawili wa Azam FC, Yakubu Mohammed na Yahaya Mohammed, waliosajiliwa kutoka timu hiyo katika usajili wa dirisha dogo.
Mbali na kufundisha soka nchini Ghana pia amewahi kufanya kazi kwenye miamba ya Morocco, Raja Casablanca, Al Masry ya Misri na katika nchi za Romania, Kuwait, Oman na Jordan.

No comments:

Post a Comment

Pages