HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 05, 2017

POLISI WAFANYA MSAKO MKALI KUWASAKA MAJAMBAZI

Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro akionesha kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, bastola aina ya Berreta iliyokamatwa kutoka kwa mlinzi wa Kampuni ya Amadori, Anwaz Ally, baada ya kubainika imefutwa namba na mtuhumiwa hana kibali cha kumiliki silaha hiyo. (Picha na Loveness Bernard).

Dar es Salaam, Tanzania

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema linaendelea kuwasaka majambazi wawili waliokimbia katika tukio lililotokea juzi ambao majambazi watatu waliua.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa 5 asubuhi katika maeneo ya Mikocheni mtaa wa Kiko Jengo la White Star Tower ambapo majambazi hao takribani watano walifika eneo hilo kwa ajili ya unyang’anyi kwenye ofisi moja ya jengo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro alisema majambazi hao ambao inasadikiwa ndio waliohusika na wizi wa milioni 26 Tazara, waliwekewa mtego na askari polisi baada ya kupata taarifa ya uwepo wao katika eneo hilo.

“Awali majambazi hao waliwekewa mtego na askari polisi baada ya kupata taarifa ya uwepo wao katika hilo…walikuwa ni majambazi watano ambao walihusika na wizi wa milioni 26 pale Tazara, katika majibizano watatu walifariki wakati wanapelekwa hospitali na wengine walikimbia pamoja na pikipiki, hivyo tunaendelea kuwasaka,” alisema.

Alisema katika tukio hilo walifanikiwa kukamata bastola mbili, moja aina ya SIG SAUER namba P 229 ikiwa na risasi nne ndani ya magazine pamoja na risasi 27.

Katika tukio lingine, Jeshi hilo limefanikiwa kukamata bastola moja aina ya Berreta na risasi 23 maeneo ya Tundwi Songani Kata ya Pemba Mnazi, Kigamboni.

“Silaha hiyo ilipatikana baada ya kupekuliwa maungoni mtuhumiwa mmoja aitwaye Anwaz Ally(45) mlinzi wa kampuni ya Amadori, katika uchunguzi silaha hiyo ilibainika kuwa imefutwa namba na mtuhumiwa huyu hana kibali cha umiliki wa halali,” alisema Sirro.
Aidha Jeshi hilo linawashikiria watuhumiwa wawili ambao ni Siasa Nassoro(28) mvuvi na mkazi wa Buyuni pamoja na Ally Omary(35) kwa kosa la kupora mali mbalimbali za watalii.

Alisema tukio hilo lilitokea Januari 4, mwaka huu ambapo katika ufuatiliaji wa tukio hilo, ndipo waliwakamata maeneo ya Buyuni wakiwa na simu 2, Solar power moja aina ya Blakbox, GPS aina ya Garmin rangi nyeusi, USB, remote control, Memory card 3, Adapter 2, betri za aina mbalimbali 11 pamoja na stendi za camera, simu na filimbi.

“Katika mahojiano na watuhumiwa hao walikiri kuhusika katika tukio hilo la uporaji wa vitu hivyo katika kisiwa cha Mapanya na kuwa walishirikiana na wenzao wengine wapatao nane ambapo msako mkali unaendelea ili kuwatafuta watuhumiwa hao wengine na wakipatikana watafikishwa mahakamani kwa hatua kali zaidi,” alisema Sirro. Jengo la White Star Tower.

Akizungumzia ajali za barabarani, alisema zimeongezeka kwa asilimia 35 ambapo katika kipindi cha Januari mpaka Desemba mwaka juzi zilitokea ajali 3710 na Januari hadi Desemba 2016 zilitokea 5719.

Alisema mwaka 2015 vifo vilikuwa 316 na mwaka 2016 vilikuwa 325 sawa na ongezeko la asilimia 2.7.

Kwa upande wa makosa ya usalama barabarani, Sirro alisema kuna ongezeko la makosa 382,207 kwani Januari hadi Desemba 2016 yalikamatwa makosa 769,170 yaliyoingizia serikali kiasi cha sh. 23,065,020,000 ukilinganisha na makosa 386,963 yaliyoingizia serikali kiasi cha 11,608,700,000 mwaka 2015 sawa na ongezeko la asilimia 49.6.

No comments:

Post a Comment

Pages