HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 06, 2017

Ujenzi wa Bararabara za juu (Flyovers) wafikia asilimia 19

Na Adili Mhina, Dar es Salaam

Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Tume ya Mipango imefanya ziara katika Mradi wa ujenzi wa Barabara za juu (Flyovers) unaoendelea katika makutano ya barabara za Nyerere/Mandela Jijini Dar es salaam na kuelezwa kuwa utekelezaji wake umefikia asilimia 19.2.

Ziara hiyo iliyofanyika hivi karibuni kwa lengo la kuangalia maendeleo ya mradi huo ilitoa fursa kwa Bw. Kiyokazu Tsuji, Mhandisi Mkazi kutoka Kampuni ya ujenzi ya Sumitomo Mitsui ambayo ndiyo inayotekeleza ujenzi huo kueleza maendeleo ya ujenzi kwa wataalam kutoka Tume ya Mipango. 

Mhandisi huyo alieleza kuwa malengo ya awali yalielekeza kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Novemba 2016, utekelezaji uwe umefikia asilimia 21.2 lakini lengo hilo halikufikiwa kutokana na moja ya mashine kupata hitilafu na kulazimika kuagiza wataalam kutoka nje ya nchi kuja kuifanyia matengenezo. 

Hata hivyo Mkandarasi huyo alieleza kuwa tayari wamejipanga vizuri katika kuhakikisha wanafidia muda uliopotea wakati mashine hiyo ilipokuwa haifanyi kazi ili ujenzi wa barabara hizo ukamilike ndani ya muda uliopangwa. 

Nao walaalam kutoka Tume ya Mipango walieleza kuwa Serikali na Wananchi kwa ujumla wanatarajia kuwa ujenzi huo utakamilika kwa muda uliopangwa hivyo Mkandarasi huyo ana wajibu wa kufanya kila linalowezekana ili mradi huo ukamilike kwa wakati. 

Wataalamu hao pia walimshauri Mkandarasi huyo kuwa ni vyema akawapeleka nje wataalam wanaoziendesha mashine hizo ili waweze kupata ujuzi na uwezo wa kutengeneza mitambo pale inapohitajika badala ya kusubiri watu kutoka nje kuja kufanya kazi hiyo. 

Walieleza kuwa kuwepo kwa wataalam wa ndani wenye uwezo wa kutatua hitilafu zinazojitokeza katika mitambo itasaidia kupunguza gharama na kuokoa muda ili kufanya mradi uende bila kusimama.

Ujenzi huo unaotekelezwa kwa miezi 35 kauanzia Disemba 1, 2015 hadi Oktoba 31, 2018 unalenga kupunguza tatizo la msongamano wa magari na kuboresha huduma za usafiri katika Jiji la Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Pages