HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 05, 2017

WAZIRI MKUU AKAGUA GHALA LA NFRA SONGEA

*Aagiza akiba iliyopo itunzwe hadi msimu ujao wa mavuno
* RC, Ma-DC, Ma-DED waagizwa kuelimisha umma utunzaji wa chakula

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua maghala ya nafaka yanayomilikiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Songea na kuagiza akiba ya mahindi iliyopo iendelee kutunzwa hadi msimu ujao wa mavuno.

Ametoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Januari 4, 2017) wakati akizungumza na baadhi ya watumishi wa NFRA Kanda ya Songea pamoja na viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma mara baada ya kukagua akiba ya nafaka iliyomo kwenye maghala ya kituo hicho.

Waziri Mkuu alisema mabadiliko ya tabia nchi yamefanya mvua zichelewe kunyesha katika mikoa mingi nchini ukiwemo mkoa wa Ruvuma ambao kwa kawaida mwezi Januari mvua ya kutosha inakuwa imeshanyesha na huwa kuna baridi nyingi.

“Angalieni ninyi wenyewe hali ya joto iliyopo hivi sasa, kwa kawaida mvua ingeshaanza kunyesha mwezi huu na mahindi yangekuwa yameanza kurefuka. Lakini hadi leo (jana) naambiwa mvua imenyesha mara mbili tu na mahindi yaliyopandwa yameanza kunyauka.”

“Kama mvua haijanyesha hadi leo, ni lazima tuchukue tahadhari, na hata mvua ikija hatujui itaendelea kunyesha hadi lini na kwa kiasi gani. RC, Ma-DC na ma-DED toeni elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa akiba ya chakula. Waambieni waachane na ngoma za unyago na sherehe za kipaimara ambazo hutumia kiasi kikubwa cha chakula,” alisisitiza.

“Msiruhusu kutoa mahindi yaliyopo na kuyauza. Hizo tani 10,500 zilizopo ziendelee kuhifadhiwa hadi tutakapoamua vinginevyo,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa NFRA Kanda ya Songea, Bw. Majuto Chabruma alimweleza Waziri Mkuu kwamba msimu huu walipanga kununua tani 22,000 za mahindi kutoka kwa wakulima lakini hadi kufikia Desemba 31, 2016, wamefanikiwa kununua tani 10,335.3 zenye thamani ya sh. bilioni 5.28.

Alisema kanda ya Songea ni miongoni mwa kanda saba zilizo chini ya NFRA ambayo inahudumia mkoa wa Ruvuma. Alizitaja kanda nyingine zinazohudumia mikoa yote nchini kuwa ni Arusha, Kipawa, Dodoma, Shinyanga, Makambako na Sumbawanga.

“Kanda ya Songea inayo maghala sita yenye uwezo wa kuhifadhi ytani 29,000 za nafaka. Lakini hivi sasa kanda hii imeingizwa kwenye Mpango wa Kuongeza Uwezo wa Hifadhi (NFRA Storage Expansion Project) na lengo la Wakala ni kufikia uwezo wa kuhifadhi tani 700,000 ifikapo mwaka 2020,” alisema.

“Kanda ya Songea tumenunua viwanja viwili vyenye ukubwa wa mita za mraba 16,986 ambapo zitajengewa silos 12 zenye uwezo wa kuhifadhi tani 46,000 na maghala mawili yenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 kila moja na hivyo kuwa na ongezeko la tani 56,000 mradi huu utakapokamilika.”

Alisema kukamilika kwa mradi huo, kutaiwezesha kanda ya Songea kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 85,000 ndani ya maghala na vihenge kutoka tani 29,000 za sasa.

Alipolizwa ni kwa nini hawajaweza kutimiza tani zote walizojipangia kununua, Bw. Chabruma alisema kuimarika kwa barabara za mkoa huo kumetoa changamoto kwa wakala kwani wananchi walianza kuuza mahindi kabla ya msimu wa ununuzi haujaanza (kawaida ni Julai mosi kila mwaka).

“Kuimarika kwa barabara za mkoa kumesaidia kufungua biashara na mikoa ya jirani na hivyo kuwawezesha wakulima wa Ruvuma kupata soko nje ya mkoa kabla NFRA haijaingia sokoni na kuanza kununua nafaka kwa wakulima vijijini,” alifafanua.

Alisema changamoto nyingine inayowakabili ni ubora hafifu wa nafaka kutoka kwa wakulima ambao alisema ni tatizo tangu hatua za awali za uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. “Ubora hafifu wa zao la mahindi ulionekana zaidi kwenye nafaka zilizooza, punje zilizovunjika, wadudu hai, rangi mchanganyiko na takataka,” alisema.

Waziri Mkuu leo anatembelea wilaya ya Songea na kukagua kituo cha kupoozea umeme katika kijiji cha Mtepa, atakagua kituo cha afya cha Madaba ambako pia atazungumza na watumishi wa ummakatia sekondari ya Madaba kabla kuhutubia mkutano wa hadhara. Pia atakagua shamba la miti la TFS katika kijiji cha Wino.

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
ALHAMISI, JANUARI 5, 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages