HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 05, 2017

WAZIRI MKUU AONGOZA MAMIA KUMZIKA KAPTENI MHAIKI

 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  na mkewe Mery Majaliwa wakiweka shada la maua katika kaburi la aliye kuwa Mkuu wa ndege za serekali Kapteni  Kenan Mhaiki  aliye fariki tarehe 31/12/2016 nakuzikwa tarehe 4/1/2017 kijijini kwao Matogoro Mkoani Ruvuma. (Picha na Chris Mfinanga).
Mke wa Marehemu  Kapteni Kenan Mhaiki  akiweka shada la maua katika kaburi la mume wake
Watoto wa Marehemu Kapteni Kenan Muahiki wakiweka Mashada ya maua katika kaburi la Baba yao.

Ruvuma, Tanzania


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameongoza mamia ya wakazi wa mji wa Songea na kata ya Matogoro kuuaga mwili wa aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), Kapteni Keenan Mhaiki katika ibada iliyofanyika kwenye parokia ya Mt. Teresia wa Mtoto Yesu iliyoko Matogoro, mjini Songea.

Waziri Mkuu ambaye ameshiriki msiba huo kwa niaba ya Serikali, pia alishiriki mazishi ya Kapteni Mhaiki ambaye pia alikuwa rubani wa ndege za Serikali yaliyofanyika kwenye makaburi ya parokia ya Matogoro.

Akizungumza kwenye ibada ya mazishi mara baada ya kutoa heshima za mwisho, leo jioni (Jumatano, Januari 4, 2017), Waziri Mkuu aliwasilisha salamu za rambirambi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan.

“Msiba huu ni wetu sote na umetugusa wote. Ni msiba mzito kwa wanafamilia na kwa Serikali pia. Kapteni Mhaiki amekuwa rubani wa ndege za Serikali kwa muda mrefu na amewaendesha viongozi wa kitaifa kuanzia awamu ya kwanza hadi awamu ya tano. Kwa niaba ya Serikali tunawapa pole sana,” amesema.

“Ninawaomba wafiwa wote hasa mke wa marehemu na watoto tushikamane katika kipindi hiki na tuendelee kuwa wavumilivu huku tukimuombea Baba yetu apate pumziko la milele,” amesema.

Kapteni Mhaiki alifariki dunia Desemba 31, 2016 katika hospitali ya Agha Khan jijini Dar es Salaam. Alilazwa katika hospitali hiyo, kabla ya sikukuu ya Krismasi, kwa ugonjwa wa saratani ya ini.

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU

No comments:

Post a Comment

Pages