HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 06, 2017

WAZIRI MKUU AZINDUA MRADI WA MAJI MADABA

*Wagharimu sh. bilioni 1.092, unahudumia wakazi 5,300

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua mradi wa maji safi na tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 200,000 ambao utahudumia vijiji viwili vya Mkongotema na Magingo katika kata ya Mkongotema, wilayani Songea, mkoani Ruvuma.

Akisoma taarifa ya mradi huo kwa Waziri Mkuu jana (Alhamisi, Januari 5, 2017), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Madaba, Bw. Shafi Mpenda alisema mradi huo ulioanza kujengwa mwaka 2013, umegharimu sh. bilioni 1.09.

“Hadi kukamilika kwake, mradi huu umegharimu sh. 1,092,439,812 ambapo kati ya hizo sh. 1,069,647,312 zimetolewa na Serikali kuu na sh. 22,792,500 zimechangwa na wananchi,” alisema.

Bw. Mpenda alisema mpaka sasa kaya 915 zenye watu 5,300 zinahudumiwa na mradi huo wenye vituo 57 vya kutolea huduma za maji kwa jamii. Alisema lengo lao ni kufikisha vituo 71 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Akifafanua zaidi, Bw. Mpenda alisema kukamilika kwa mradi huo kumesaidia kuwapunguzia wananchi gharama za kununua maji ambapo pipa moja liligharimu sh. 3,000. “Pia kutasaidia kupunguza adha ya kufuata maji umbali mrefu; kupunguza magonjwa yanayotokana na mlipuko na kuwapa wananchi muda wa kutosha kufanya shughuli nyingine za maendeleo,” alisema.

Akizungumza na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa mradi huo, Waziri Mkuu aliwapongeza wakazi hao kuwa kukubali kuchangia ujenzi wa mradi huo kwani katika baadhi ya maeneo miradi kama hiyo imekwama kukamilika kwa sababu wananchi waligomea kuchangia.

Aliwataka wakazi wa vijiji hivyo wasiharibu mazingira na watunze vyanzo vya maji ili mradi huo uweze kuwa endelevu. “Mradi huu ni lazima tuutunze kwani hali ya hewa imebadilika sana hivi sasa, sababu ni sisi wenyewe wananchi ambao tumekata miti sana ili kupanua maeneo ya kilimo.”

“Changamoto inayotupata hivi sasa ni kwama tumebakia kuwa na eneo kubwa la kilimo lakini mazao yanayopatikana ni kidogo. Mtazamo wetu katika Serikali hivi sasa ni kulima kwenye eneo dogo lakini mavuno yawe mengi,” alisema.

“Mtu asilime chochote karibu na chanzo hiki ili tuweze kukitunza chanzo chetu. Na wenyeviti wa Serikali za vijiji vyote viwili, wekeni utaratibu wa wananchi kwenda kupanda miti ili eneo hili libaki kuwa na unyevunyevu kwa muda mrefu,” alisisitiza.

“Sera ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata maji katika umbali usiozidi mita 400, na hili tutaweza kulitimiza kama tu mtatunza vyanzo vya maji vilivyopo,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kuwaomba wakazi wa vijiji hivyo watunze akiba ya chakula walichonachi kwa sababu hali ya hewa imebadilika na hakuna anayejua mvua itaanza kunyesha lini. “Hatujui mvua itakuja lini na kwa kiasi gani; mara zitakapoanza kunyesha kila mmoja katika familia ahakikishe analima mazao mbadala kama kunde, maharage na mihogo ambayo yanastahimili ukame,” alisema.

Waziri Mkuu pia alikagua utoaji huduma kwenye kituo cha afya cha madaba na ujenzi wa kituo cha kupozea umeme cha Madaba.

IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
IJUMAA, JANUARI 6, 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages