HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 12, 2017

WAZIRI MKUU AZINDUA SACCOS YA MELINNE

*Awataka viongozi kuwa wawazi
*Awashauri kuanzisha viwanda

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Melinne saccos kuhakikisha wanakuwa wawazi na kutoa taarifa za hesabu za umoja huo kila wakati ili wanachama waweze kuwa na takwimu sahihi.

Alitoa agizo hilo jana jioni (Jumatano, Januari 11, 2017) wakati akizindua saccos hiyo yenye mtaji wa zaidi ya sh. bilioni moja kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinguzi Matukufu ya Zanzibar.

Waziri Mkuu alisema viongozi hao wanatakiwa kuwa wawazi kwa wanachama wenzao jambo ambalo litawajengea uaminifu hivyo kuwezesha umoja huo kudumu na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Alisema vyama vingi vya ushirika nchini vimekufa kutokana na viongozi wake kutokuwa waaminifu hivyo Serikali hatokubali kuona suala hilo linatokea katika umoja huo kwani litakwamisha maendeleo.

Aidha, Waziri Mkuu aliwapongeza wananchi hao kwa kuanzisha saccos hiyo kwani wameweza kutimiza ndoto ya Rais wa kwanza wa Zanzibar Hayati Sheikh Abeid Amani Karume ya kuondokana na umasikini, dhuluma na unyonge.

Waziri Mkuu alisema saccos hiyo itawawezesha baadhi ya wanachama kuanzisha miradi ya ujasiriamali na wengine kuongeza mitaji hivyo kukuza biashara zao na kuondokana na umasikini.

Awali, Waziri Mkuu alizindua ukumbi wa kisasa wa mikutano unaomilikiwa na saccos hiyo na kuwapongeza wananchi hao kwa kubuni miradi ya maendeleo itayowaongezea kipato na kuweza kujikwamua kiuchumi.

Hata hivyo aliwataka wanachama hao kuendeleza mshikamano wao na kuendelea kushirikiana na Serikali ambayo imejipanga kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutoa mikopo ya ujasiriamali hasa kwa walio katika vikundi vya uzalishaji.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliwashauri wanachama wa umoja huo kufikiria uwezekano wa kuanzisha viwanda ili kukuza mitaji yao. Pia vitawezesha umoja kuongeza za fursa za ajira nchini.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMIS, JANUARI 12, 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages