HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 22, 2017

Askofu Gadi Ampongeza Rais magufuli kwa Kumteua Kamishna wa Kupambana na Dawa za Kulevya

 Maaskofu wa Madhehebu mbalimbali wakimuombea Rais Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika ukumbi wa Idara ya Habari -MAELEZO,leo Jijini Dar es Salaam.
Maaskofu wa Madhehebu mbalimbali nchini wakiongozwa na Askofu wa Good News for All Ministry  Dkt. Charles Gadi (wa tatu kutoka kushoto) wakiombea Bendera ya Tanzania ili Amani iendelee kutawala.

Na Lilian Lundo – MAELEZO

Askofu wa Good News  for All Ministry  Dkt. Charles Gadi  kwa niaba ya dini na madhehebu mbalimbali hapa nchini wamempongeza  Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumteua Kamishna wa Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.

Dkt. Gadi ametoa pongezi hizo leo, Jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na vyombo vya habari katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO).

“Tunamshukuru Mungu kwa kumuinua Rais ambaye ameonyesha nia na kuwa mstari wa mbele  kupigana na biashara hiyo haramu, ni ukweli usiopingika kwamba tatizo la dawa  ya kulevya ni kubwa na lenye madhara makubwa sana kwa watanzania  wengi haswa vijana ambao ni nguvu kazi  ya Taifa,” alifafanua Dkt. Gadi.

Aliendelea kwa kusema kuwa, Vijana wengi wamepoteza maisha , kuharibika akili, kupata magonjwa ya kuambukiza, kupoteza  malengo ya kimaisha kwa sababu ya dawa hizo. Vile vile dawa hizo zimeleta fedheha kwa Taifa kutokana na Vijana wengi wa Kitanzania kuwepo katika magereza mbalimbali Duniani huku wengine wakisubiri adhabu  ya kunyongwa.

Aidha amempongeza Rais Dkt. Magufuli kwa kuimarisha Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa  kumteua Kamishna ambaye atasimamia Mamlaka hiyo na anaamini kwamba kwa neema ya Mungu ataweza kumsaidia kikamilifu  Rais Magufuli katika kutimiza azma yake ya kukomesha  biashara hiyo.

Wakati huo huo, Dkt. Gadi amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuianzisha vita hiyo dhidi ya matumizi ya dawa kulevya katika mkoa wa Dar es Salaam. Vile vile amewapongeza waandishi wa habari na vyombo mbalimbali vya habari kwa kutoa habari zinazosaidia katika upambanaji wa  biashara hiyo.

Dkt. Gadi amewataka viongozi wa Dini kuungana bega kwa bega na Rais Magufuli kwa kuendelea kutoa maadili kwa vijana ili kuepukana na uovu wa dawa za kulevya nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages