HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 20, 2017

PAMBANO LA SIMBA NA YANGA SERIKALI YATOA TAMKO

Ofisa Usalama Viwanjani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), anayetambuliwa na FIFA, Inspekta Hashim Abdallah akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu namna jinsi Jeshi la Polisi lilivyojipanga kuimarisha ulinzi na usalama wakati wa mechi ya Simba na Yanga Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. (Picha na Francis Dande).


Ndugu Watanzania Jumamosi, tarehe 25/02/2017 saa 10.00 jioni Uwanja wa Taifa tutakuwa na mchezo mkubwa wa kati ya Simba SC na Yanga FC.

Ikumbukwe kuwa mchezo uliopita wa timu hizi uliochezwa kwenye uwanja huu tarehe 1/10/2016 zilitokea vurumai zilizosababisha Serikali kuufungia Uwanja kwa zaidi ya miezi mitatu. Vurugu hizo zilisababisha uharibifu wa miundombinu ikiwemo uvunjifu wa viti, mageti na mbaya zaidi baadhi ya watu walijerehuliwa.

Tunaomba waandishi na wadau wote tushirikiane kuelimisha umma wa wapenda michezo kuwa Michezo ni Furaha, Amani na Upendo.

Kuelekea mchezo ujao tungependa kueleza yafuatayo:-
Tunawaomba wadau wote tujenge utamaduni wa kununua tiketi mapema kwani mpaka sasa tiketi zinapatikana kupitia SELCOM. Hii itaondoa msongamano na lawama zisizo za lazima.

Tunafahamu kuwa kuna changamoto za matumizi ya mfumo wa Ki- elektroniki lakini hatuna budi kuendelea kuelimishana na kujifunza kwani huko ndiko Dunia ilipo,tutakua watu wa ajabu leo tukisema hatuwezi kutumia mfumo huu kisa changamoto hizi ndogondogo zinazojitokeza.

Tujiepushe na vurugu za aina yoyote siku ya mchezo kwani Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayepelekea uvunjifu wa amani siku ya mchezo.

Kutakua na ulinzi wa kutosha ndani na nje ya Uwanja hasa ukichukulia kuwa kuna kamera zenye uwezo wa kumuona kila mtu anayeingia Uwanjani na kila anachokifanya. Tutapiga picha na kuzirusha kwenye TV kubwa ya Uwanja kwa wale wote watakaobainika kuashiria/kutenda vurugu sheria itachukua mkondo wake.

Tunatoa rai kwa      waamuzi waliopewa dhamana ya kuchezesha mchezo huu,wajue kuwa wana dhamana kubwa hivyo ni vyema wakafuata kanuni na sheria za mchezo husika ili kuepusha malalamiko.

Mwisho napenda niwatakie mchezo mwema kwa timu zote wajue kuwa Watanzania wanategemea burudani nzuri kutoka kwao,na niwaombe mashabiki wakumbuke kuwa wajibu wao mkuu ni kuzishangilia na kuzipa hamasa timu zao na si vinginevyo.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, Boniface Wambura yeye kwa upande wake, alisema kwamba mchezo huo utaanza saa 10.00 jioni na kwamba mwamuzi atatangazwa wakati wowote kuelekea mchezo huo.

Alionya mashabiki kutofanya vurugu kwa sababu masharti ya kuufungulia yanakwenda sambamba na kuchunguzwa kama jamii ya wapenda soka kama imejirekebisha baada ya kutokea vurugu Oktoba mosi, mwaka jana.

Mtoa Huduma wa Mauzo ya Tiketi
Meneja Mauzo wa Kampuni inayotoa Huduma ya Kuuza Tiketi za Elektroniki, Gallus Runyeta alisema kwamba wanatarajiwa kutoa huduma ambayo haitakuwa na changamoto kama ilivyotokea huko nyuma.

Ofisa Usalama wa TFF/FIFA
Ofisa Usalama wa TFF/FIFA, Inspekta Hashim Abdallah, alisema kwamba Jeshi la polisi limejipanga vema kudhibiti kila aina ya fujo zinazoweza kujitokeza kwani wana askari kama 300.

..…………………………………………………………………………........................


IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments:

Post a Comment

Pages