HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 17, 2017

Maafisa Habari na Mawasiliano wa Serikali Watoa Misaada Shule ya Msingi Buigiri Wasioona

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari (Maelezo), Zamaradi Kawawa, akikabidhi moja ya mashine za nukta nundu kwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Buigiri iliyopo Mjini Dodoma. (Picha na Raymond Mushumbusi-WHUSM).

Na Lilian Lundo – MAELEZO

Maafisa Habari na Mawasiliano wa Serikali wametoa misaada ya vifaa vya kufundishia, kujifunzia pamoja na vyakula kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Buigiri Wasioona iliyopo wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Akikabidhi vifaa na vyakula hivyo kwa wanafunzi hao kwa niaba ya Mkurugenzi Idara ya Habari (MAELEZO) Dkt. Hassan Abbasi, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara  hiyo, Zamaradi Kawawa alisema kuwa wamewiwa kutoa misaada kwa wanafunzi hao ili waweze kujifunza vema na kufikia malengo yao.

“Kila mwaka tunapokutana katika mkutano wa Maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini huwa tunatembelea watu wenye mahitaji mbalimbali na kutoa misaada. Kwa mwaka huu tumefanya mkutano wetu hapa Dodoma, hivyo tumeona misaada yetu tuilete Shule ya Msingi Buigiri Wasioona,” alifafanua Zamaradi Kawawa.

Akifafanua zawadi zilizotolewa Zamaradi alisema kuwa Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO)  kwa kushirikiana na Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo wametoa msaada wa mashine Nne za nukta nundu (Perkins Brailler Machine), Rimu 40 za karatasi za kuchapa nukta nundu (Brailler Paper), Mchele, Maharage, Sukari, Unga na Juice.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Samwel Jonathan amewashukuru Maafisa Habari hao kwa msaada waliotoa na kusema utatua kwa kiasi kikubwa changamoto za ukosefu wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia shuleni hapo.

Mwalimu Samwel Jonathan amesema, licha ya shule hiyo kuwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa mashine za nukta nundu, viti, meza pamoja na uchakavu wa madarasa na majengo lakini shule hiyo imekuwa ikifaulisha wanafunzi wake kwa asilimia 100 katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi kwa zaidi ya miaka kumi sasa.

Vilevile amesema shule hiyo inapokea fedha toka Serikalini ikiwa ni utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo  ambayo hutumika kununua chakula na uendeshaji wa kila mwezi shuleni hapo. Ambapo kwa mwaka wa fedha 2016/17 shule hiyo imepokea shiligi 150,000,000 kwa ajili ya maendeleo ya shule.

Akitoa shukrani ya misaada waliopokea shuleni hapo mwanafunzi Joseph Richard amesema elimu ndio msingi wa maisha hivyo na wao wanahitaji elimu kama ambavyo watoto wasio na ulemvu wanavyohitaji. Aidha, alishukuru kwa misaada iliyotolewa na kuwaombea baraka wote waliofanikisha kupatikana kwa misaada hiyo.

Shule ya Msingi Buigiri Wasioona ni miogoni mwa shule Kongwe nchini, ambayo ilianzishwa Aprili 30, 1950 na Mzungu aliyeitwa Captain Fred Valley  ambapo ilikuwa ikiongozwa na kumilikiwa na kanisa la Anglikani ikiwa na lengo la kuwawezesha watu wazima wasioona wajue kusoma neno la Mungu.

Baada ya nchi kupata uhuru mwaka 1961 Serikali iliamua kushirikiana na kanisa katika kuendesha shule hiyo, ambapo mpaka sasa shule hiyo inahudumiwa na Serikali na Kanisa.

Shule hiyo ni ya bweni na kutwa ambapo  ina jumla ya wanafunzi 115, wavulana 70 na wasichana 45  wakiwa wamechanganywa na wanafunzi wasio walemavu ambao hawazidi wanafunzi 31 ili wanafunzi wenye ulemavu wasijione kuwa wanatengwa.

No comments:

Post a Comment

Pages