HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 24, 2017

MSAMA: Tamasha la Pasaka ni zaidi ya kuimba, kushiriki


.Asema ni kielelezo cha umoja wa Watanzania
.Ni faraja kwa wenye ulemavu, yatima, wajane

Na Mwandishi Wetu

WENGI wamelisikia ama kuliona tukio la Tamasha la Pasaka ambalo limekuwa likifanyika kila mwaka tangu mwaka 2000, chini ya uratibu wa Kampuni ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam.

Tukio hili ambalo msingi wake ni kueneza injili ya mungu kupitia sauti, magitaa, ngoma, vinanda na pachanga, pia limekuwa likibeba malengo mengine kuntu.

Katika mahojiano na Mkurugenzi wa Msama Promotions Ltd inayoratibu tukio hilo na mengineyo ya muziki wa Injili kama Krismasi na uzinduzi wa kazi za waimbaji mbalimbali, anayachambua malengo hayo moja baada ya jingine.

Neno la Mungu

Msama anasema nyimbo za Injili zimejaa habari kamili ya neno la Mungu ambalo hufikishwa kwa wanadamu kwa njia ya uimbaji iwe katika ukumbi ama uwanjani, hivyo uimbaji ni mahubiri kamili ya neno la Mungu ambao hufikishwa kirahisi.

Anasema wakati anapata wazo la kuanzisha Tamasha la Pasaka, lengo kuu hasa lilikuwa hilo la kufikisha ujumbe wa neno la Mungu kwa wengine kwa njia ya kuwaleta pamoja waimbaji na kumtukuza Mungu kwa sauti na vinanda.

Hata hivyo, Msama anasema katikati ya lengo hilo la msingi ambapo katika miaka ya awali ilikuwa kazi ngumu mno kutokana na muziki wa Injili kutokuwa maarufu kama ilivyo sasa, ikajitokeza fursa nyingine sambamba na lengo hilo.

Makundi maalumu

Msama anasema lengo jingine ambalo likajitokeza kwa waratibu wa tamasha hilo ni kutumia kidogo kinachopatikana kufariji makundi maalumu katika jamii kama walemavu, wajane na yatima.

Imekuwa hivyo kila mwaka kwa Msama Promotions Ltd iwe kabla ama baada ya Tamasha la Pasaka, kuona inatoa msaada kwa vituo vya kelelea yatima pamoja na kutoa misaada ya vitu kadha wa kadha kwa wajane na walemavu.

Msama amekuwa akisisitiza kuwa wamekuwa wakitimiza wajibu huo kwa kusaidia makundi maalumu kwa sababu ni jambo jema  ambalo limesisitizwa pia katika vitabu vitakatibu.


Msingi wa umuhimu wa kusaidia makundi hayo maalumu, ni kutokana kuwa wahushika wameangukia katika uyatima, ulemavu ama ujane, hivyo wanahitaji kila aina ya sapoti kutoka kwa jamii.

Kukuza muziki wa Injili

Msama anasema uwepo wa Tamasha la Injili, kwa kiasi kikubwa limechangia kukua kwa muziki huo wa injili ambao leo hii ni maarufu hadi kuwa biashara na ajira kwa vijana wenye vipaji.

Anasema vipaji anavyozungumzia si vya kuimba na kupamba jukwaa, pia hata wale watengenezaji wa muziki achilia mbali watu waliofungua maduka ya kuuza kazi za waimbaji, wengine wamekuwa wakitembeza mitaani.

Msama anasema wao wanajisikia fahari kuona juhudi zao za kueneza neno la Mungu kupitia Tamasha hilo, zimezidi kufanikiwa ambapo muziki wa Injili sasa unapigwa kila kona bila kujali tofauti za dini zilizopo katika jamii.

Kiunganishi cha dini zote

Msama anasema hiyo inatokana na msingi ambao wao waratibu wameujenga tangu kuanza kwa tamasha hilo miaka 17 iliyopita ambapo kigezo cha udini kiliwekwa kando wakati wa kuteua mgeni rasmi.

“Ingawa Pasaka ni tukio la Kikristo, lakini tamasha hili limekuwa kielelezo cha umoja wetu kitaifa kwa sababu tumekuwa na viongozi mbalimbali ambao wamewahi kupewa dhamana ya kuwa wageni rasmi na kuwa kivutio kikubwa.

“Nakumbuka mzee wetu Rais mstafu Ali Hassan Mwinyi, amewahi kuwa mgeni rasmi, Rais  wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete pia amewahi kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Pasaka na wengineo wengi tu na wakawa baraka,” anasema.

Jukwaa la waimbaji

Kwa upande mwingine, Tamasha la Pasaka limekuwa kama kioo cha muziki wa Injili tangu mwaka 2000 ambapo waimbaji mbalimbali wa ndani wamekuwa wakitamani kupata nafasi ya kuimba kuonyesha uwezo ama kutambulisha kazi.

“Hakuna ubishi, uwepo wa Tamasha la Pasaka kumesaidia kuibua vipaji vipya vya muziki wa Injili ambavyo leo hii vimezidi kutesa kama Rose Muhando, Bonny Mwaitege, Matha Mwaipaja, Faraja Ntaboba na wengine wengi maarufu leo,” anasema Msama.


Kielelezo cha ushirikiano

“Mbali ya kuibua vipaji, pia Tamasha la Pasaka limekuwa kama kiunganishi cha waimbaji wa ndani na wale wa nchi nyingine ambapo kila mwaka waimbaji kutoka Afrika Kusini, Rwanda, Zambia na DR Congo na Kenya hualikwa,” anasema.

Kati ya waimbaji waliowahi kualikwa ni Rebecca Malope, Solly Mahlangu na Sipho Makabane  (Afrika Kusini), Ephraem Sekereti  (Zambia), Annastazia Mukabwa, Solomoni Mukubwa (Kenya), Kwetu Pazuri (Rwanda) na Ntabona (DR Congo).

“Kitendo cha Tamasha la Pasaka kusheheni waimbaji wa Tanzania na wale kutoka nje kila mwaka, kwa kiasi kikubwa kumechangia hamasa mpya ya muziki wa Injili kwani waimbaji wote wamekuwa wakibadilishana uzoefu na vionjo vya uimbaji.”


 Ajenda mahususi

Mbali ya malengo yake ya msingi, pia Tamasha la Pasaka limekuwa likitumika kubeba ajenda mbalimbali kulingana na mahitaji ya wakati husika kwa mfano, wakati wa matatizo, limekuwa likitumika kumwomba Mungu aisaidie nchi.

Msama anasema kama ni  mwaka wa uchaguzi, tamasha hilo pia limekuwa likibeba ajenda ya kuliombea taifa lipite salama katika tukio hilo ambalo kwa baadhi ya nchi limewahi kuacha machafuko na uhasama mkubwa wa kisiasa.

Anatoa mfano, ajenda ya tamasha la mwaka huu litakalozinduliwa  Aprili 16 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, ni kuiombea serikali iliyopo madarakani iweze kufanikiwa katika malengo yake ya kuiletea nchi mafanikio mbalimbali.

Kuhusu maandalizi ya tukio la mwaka huu, Msama anasema yamekamilika kwa asilimia 90 kwani waimbaji wamezidi kuthibitisha ambao ni Christina Shusho, Martha Mwaipaja, Jesca ‘BM’ na Godluck Gosbert, moja ya waimbaji chipukizi.

Wengine ni  Kwaya ya Ulyankuru Tabora, maarufu kama Kwa Viumbe Vyote iliyowahi kutikisa vilivyo katika miaka ya 90, kutokana na kuimba nyimbo zenye ujumbe kamili wa neno la Mungu.

Kwaya nyingine ni Kinondoni Revival Choir ambayo italitumia tamasha hilo kuzindua albamu yake mpya huku malkia wa Muziki wa Injili nchini, Rose Muhando naye akitarajiwa kufyatua albamu yake ya Ruth.

Msama anasema mipango imezidi kwenda vizuri ambapo kiingilio katika viwanja vyote litakapofanyika tamasha hilo, viti maalumu ni shilingi 10,000 na wakubwa ni Sh 5,000 na watoto ni shilingi 3,000.

Anasema wameamua kupanga viingilio vya kawaida kuwezesha wengi kuipata fursa hiyo ya kuona uhondo wa tamasha hilo ambali safari hii litakuwa latofauti zaidi kutokana na aina ya maandalizi wanayofanya.

Msama anasema baada ya uzinduzi wa Uwanja wa Uhuru, uhondo wa tukio hilo utaelekea Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma, Shinyanga, Simiyu, Mwanza na mwishowe Iringa.

Anatoa wito kwa wadau wa muziki wa Injili kujitokeza kwa wingi katika tamsha hilo litakapofanyika ili kuchota baraka za Mungu kupitia ujumbe wa nyimbo mbalimbali zitakazoimbwa.

“Nawaalika wadau na wapenzi wote wa muziki wa Injili ambao hauna dini, wajitokeze kwa wingi katika tamasha letu ambalo tumeliandaa kwa viwango vya kimataifa kukidhi matarajio ya wengi ambao wamekuwa wakitusapoti kila mwaka,” anasema.                                             
                                                          











  








No comments:

Post a Comment

Pages