HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 07, 2017

PROF. NDALICHAKO AZINDUA BODI MPYA YA TEA NA KUIPA MUDA

 Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiongea na wajumbe wa Bodi mpya ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) leo Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo ambapo ameielekeza Bodi hiyo kutekeleza miradi Kwa wakati.
 Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi mmoja wa wajumbe wapya wa Bodi ya Elimu Tanzania (TEA), Gerald Mweli, mwongozo wa kutekeleza majukumu ya bodi.
Wajumbe wa Bodi ya Elimu Tanzania (TEA) pamoja na watendaji wa Mamlaka hiyo wakisikiliza hotuba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo.


Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Joyce Ndalichako ameitaka Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kuanza utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya mamlaka hiyo ifikapo Juni 30.
Akizungumza na watendaji wa TEA jijini Dar es Salaam jana wakati wa kuzindua bodi ya mamlaka hiyo alisema miradi 59 iliyotengewa zaidi ya sh. bilioni 654 iliyoanza tangu mwaka 2013 inatakiwa kukamilika ndani ya muda huo.
“Napata mashaka na miradi inayokaa muda mrefu kwanza ubora wake hautakuwa mzuri. Naomba muianze na mnipeleke ‘site’ nikajionee. Pesa zipo kwanini miradi haikamiliki?.
“Inawezekana TEA mnajibebesha majukumu yasiyowahusu ndio maana hammalizi miradi yenu. Ninyi watu wa manunuzi wekeni mifumo yenu vizuri toeni nafasi kwa mnaofanya nao miradi kuwatafuta wakandarasi wao wenyewe msifanye kila kitu ninyi,” alisisitiza Waziri Ndalichako.
Waziri huyo aliitaka bodi hiyo mpya chini ya uenyekiti wa Profesa Moris Mbago kuhakikisha mradi wa nyumba 25 kati ya 40 zilizoanza kujengwa kwenye wilaya mbalimbali zinakamilika ili walimu wapate mahali pa kuishi na kuifurahia kazi yao.
“Mnapokaa vikao mnatakiwa kujitathimini mmefanya nini sio mnamipango gani… serikali ya awamu ya tano inataka hapa kazi tu na kazi lazima ionekane imefanyika sio ipo kwenye mpango wa kufanyika.
“Mwenyekiti najua pesa zipo nakuomba uhakikishe miradi inakamilika au ipo kwenye hatua za mwisho za kukamilika kwake kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha. 
“Nataka kwenda bungeni kwenye bajeti nitawaambia nini wananchi niliowaahidi nyumba za walimu? Inamaana nisiendele bungeni wakati kuna mtu anayewajibika katika hilo? 
“…Hapana naomba mniite baada ya miezi mitatu nikaione miradi iliyokamilika,” alisisitiza waziri huyo.
Akimshukuru waziri huyo, Profesa Mbago alisema bodi yake yenye wajumbe sita itashirikiana na watendaji wengine wa TEA kuhakikisha wanayafikia maelngo waliyowekewa na waziri huyo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa TEA, Graceana Shirima aliahidi kutimiza yote waliyotakiwa kufanya na waziri huku akimhakikishia watafanya kazi kwa kasi inayotakiwa na Rais John Magufuli.

No comments:

Post a Comment

Pages