HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 24, 2017

Rais Magufuli awaapisha Mawaziri wawili, Katibu Mkuu, Mabalozi sita na Kamishna Tume ya Mahakama

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 24 Machi, 2017 amewaapisha Mawaziri wawili, Katibu Mkuu Ikulu, Mabalozi wanne na Kamishna wa Tume ya Mahakama, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Walioapishwa ni Mhe. Dkt. Harrison George Mwakyembe aliyeapishwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Aidan John Mwaluko Kabudi aliyeapishwa kuwa Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, na Bw. Alphayo Kidata aliyeapishwa kuwa Katibu Mkuu – Ikulu.

Wengine ni Mhe. Sylvester Mabumba aliyeapishwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Dkt. Abdallah Possi aliyeapishwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Job Masima aliyeapishwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Israel na Mhe. Jaji Stella Esther Mugasha aliyeapishwa kuwa Kamishna wa Tume ya Mahakama.

Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi hao, Mhe. Rais Magufuli amewataka kuchapa kazi kwa juhudi, maarifa na kwa kutanguliza maslai ya Taifa na pia amewasihi kutobabaishwa na kauli ama vitendo vyovyote vya kuwavunja moyo.

Mhe. Rais Magufuli pia amewasihi waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari kufanya kazi zao kwa weledi na kwa kutanguliza maslai ya Taifa badala ya kutoa kipaumbele katika masuala ya migogoro na mambo mengine yasiyo na manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Nchi yetu huko nje ina sifa kubwa sana, juzi tu hapa amekuja Rais wa Benki ya Dunia na amekubali kutupatia Shilingi Trilioni 1.74 na pia Benki ya Dunia ipo katika mchakato wa kutupatia fedha zingine Shilingi Trilioni 2.8 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, haya ndio mambo muhimu ya kuandika lakini hebu angalia siku iliyofuata jinsi magazeti yalivyoandika” amehoji Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, amewaonya wamiliki wa vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikiandika habari za uchochezi na amemtaka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe kuhakikisha vyombo vya habari vinafanya kazi kwa kufuata sheria na havitumiwi kuvuruga nchi.

Kabla ya kuwaapisha viongozi hao, Mhe. Rais Magufuli amepokea hati za utambulisho za Mabalozi 6 walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Mabalozi hao ni Balozi wa Cyprus hapa nchini mwenye makazi yake Mjini Muscat - Oman Mhe. Andreas Panayiotou, Balozi wa Bangladesh hapa nchini mwenye makazi yake Mjini Nairobi – Kenya Mhe. Meja Jenerali Abdul Kalam Mohammad Humayun Kabir na Balozi wa Nepal hapa nchini mwenye makazi yake Mjini Pretoria – Afrika Kusini Mhe. Amrit Bahaur Rai.

Wengine ni Balozi wa Ecuador hapa nchini mwenye makazi yake Mjini Addis Ababa – Ethiopia, Balozi wa New Zealand hapa nchini mwenye makazi yake Mjini Pretoria – Afrika Kusini na Balozi wa Jamhuri ya Kongo mwenye makazi yake Mjini Kigali – Rwanda Mhe. Michael Gerrard Burrel.

Katika mazungumzo yake na Mabalozi hao Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na amewahakikishia kuwa Tanzania itaendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano na nchi hizo, huku akitilia mkazo ushirikiano katika masuala ya uwekezaji, biashara na kubadilishana uzoefu katika uzalishaji mali hususani kilimo.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
24 Machi, 2017

 Balozi wa Kongo akikabidhi hati za utambulisho kwa Rais Magufuli leo. (Picha na Francis Dande).
Rais John Magufuli, akimuapisha Dk. Harrison Mwakyembe, kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ikulu jijini Dar es Salaam.
 Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk. Abdallah Possi akila kiapo mbele ya Rais Dk. John Magufuli ikulu jijini Dar es laam leo.
 Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk. Abdallah Possi akipokea vitendea kazi kutoka kwa Rais Dk. John Magufuli ikulu jijini Dar es laam leo.
 Mawaziri wakila kiapo cha uhadilifu.
 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akizungumza baada ya kula kiapo ikulu.
 Rais John Magufuli akizungumza katika hafla ya kuapisha mabalozi na mawaziri.
 Picha ya pamoja.
 Waziri Mpya wa Sheria na Katiba, Prof. Palamagamba Aidan John Mwaluko Kabudi, akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa wizara hiyo.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akiongea na wanahabari wa vyombo mbalimbali baada ya hafla ya kuwaapisha mawaziri, mabalozi na Kamishna Ikulu jijini Dar es salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akiongea na wanahabari wa vyombo mbalimbali baada ya kuhitimisha hafla ya kuwaapisha mawaziri, mabalozi na Kamishna Ikulu jijini Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment

Pages