HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 05, 2017

Rais Magufuli ataka benki zipunguze riba

NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, amezitaka taasisi za kifedha nchini nchini, hususani benki, kupunguza riba ili kuharakisha ongezeko la Watanzania kukopa kwa manufaa na hivyo kuchangia maendeleo ya Taifa.

Rais Magufuli alitoa wito huo mwishoni mwa wiki, wakati akizindua Kituo cha Kibiashara cha NMB kilichopo Mkoani Mtwara ( NMB Mtwara Business Centre), kilichoko Mtwara Mjini.

Alizitaka benki nchini kuangalia uwezekano wa kushusha riba, huku akiwahakikishia kuwa jambo hilo litawahamasisha zaidi Watanzania kukopa benki na hivyo kutanua wigo wa makuzi ya pato na faida ya benki kibiashara.

“Naomba mabenki waanze kufikiria kupunguza riba, mkirekebisha riba zenu Watanzania wengi zaidi watahamasika kukopa na nyinyi kupata faida zaidi,” alisema Rais Magufuli ambaye hiyo ni mara yake ya kwanza kufungua tawi la NMB tangu kuingia madarakani.

Rais Magufuli pia alizitaka benki nyingine Tanzania kujikita katika kufanya biashara na wananchi kupitia mikopo, kuliko kung’ang’ania kufanya biashara na serikali tu kupitia hati fungani za serikali.

Pia aliiomba NMB kuunga mkono ajenda ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, akisema: “Naomba NMB mshiriki katika kukopesha viwanda hasa vidogo vidogo na hivyo kuunga mkono juhudi za serikali katika mchakato huo.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Profesa Joseph Semboja, alisema kuwa benki yake imefanya maboresho makubwa na hivyo kuwa na uwezo mkubwa wa kutoa huduma za kifedha kwa kila kada ya Watanzania na serikali kwa ujumla.

Prof. Semboja alisema kuwa Serikali kwa sasa inamiliki hisa asilimia 32 ndani ya benki ya NMB zenye thamani ya zaidi ya Sh. Bil. 430 hivyo kuiwezesha serikali kupata gawio la zaidi ya Sh. Bil. 75 ndani ya miaka mitano.

Mkurugenzi Mkuu wa NMB, Ineke Bussemaker, alisema kuwa nia ya benki yake ni kuendelea kukua zaidi huku ikitoa suluhu ya vipaumbele vya serikali na kujikita katika ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa njia za kielektroniki.

Kituo cha Kibiashara cha Mtwara, ni cha tisa kufunguliwa na NMB baada ya vituo vya biashara vya Mwanjelwa Mbeya, Mwanza, Makole Business Centre Dodoma, Moshi, Arusha, Morogoro na vituo vya kibiashara vya Sinza na Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya NMB Ineke Bussemaker mara baada ya kukifungua kituo hicho cha kibiashara mkoani Mtwara.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango Mtkurugenzi Mkuu wa Benki ya NMB Ineke Bussemaker wakikata utepe kuashiaria ufunguzi rasmi wa Kituo cha Biashara cha Benki hiyo mkoani Mtwara.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya NMB Ineke Bussemaker, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Halima Dendego wakipiga makofi mara baada ya kufungua kituo hicho cha Kibiashara cha NMB mkoani Mtwara. 

No comments:

Post a Comment

Pages