HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 17, 2017

RT KUENDESHA MAFUNZO YA MAKOCHA WA RIADHA KWA WATOTO-(KIDS ATHLETICS)

Na Mwandishi Wetu
KOZI maalumu ya mchezo wa riadha kwa watoto ‘Kids Athletics’ inatarajiwa kufunguliwa kesho jijini Dar es Salaam ikishirikisha washiriki 24 kutoka Tanzania Bara na Visiwani.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday, mpango huo maalumu wa kuzalisha wakufunzi wa riadha kwa watoto umewezeshwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF).

Gidabuday, alisema kozi hiyo itaendeshwa na Mkufunzi anayetambuliwa na IAAF, Dk. Ahmad Ndee na itafanyika kwa siku mbili Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

“Kozi hii ni muhimu sana katika maendeleo ya mchezo wa riadha, kwani inazalisha makocha ambao watakuwa msingi katika kutambua vipaji na kuviendeleza, kitu ambacho ndio msingi katika mchezo wowote ule, kwani vipaji vinapaswa kutambuliwa toka chini,” alisema Gidabuday.

Gidabuday, alisema kozi hiyo itafunguliwa na Makamu wa Kwanza wa Rais RT-Utawala, William Kallaghe na inatarajiwa kufungwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohammed Kiganja.

Aliwataja washiriki hao na mikoa wanayotoka kwenye mabano kuwa ni Kapteni mstaafu Lucas Nkungu, Juma Nchimbi (Dar), Michael Ligola, Faraja Makula (Pwani/Moro), Restituta Joseph, Charles Maguzo (Arusha/Manyara), Masumbuko Manyanda, Amir Sangawe (Tanga/Kilimanjaro), Winfrida Raphael, Madai Jambau (Dodoma/Singida), Catherine Mnonjela (Lindi), Simon Mgaya (Ruvuma/Njombe), Jamida Alfred, Lwiza John (Iringa, Mbeya na Songwe).

Wengine ni Esther Mloge (Tabora/Shinyanga), Nice Nkaluka, Vedastus Makaranga (Mwanza/Mara), Adam Tunga (Rukwa/Katavi), Oscar Mwaipaja (Kigoma/Kagera na Geita), Elias Ngili (Simiyu), Othman Msabaha, Mlingi Mganga Bwire (Mjini Magharibi/Kusini Unguja na Kaskazini Unguja), Talib Ali Rajab (Kusini Pemba/Kaskazini Pemba), na Alfred Mandela (FBS).

Washiriki hao wanatarajiwa kuanza kuwasili jijini Dar es Salaam leo.

No comments:

Post a Comment

Pages