HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 30, 2017

SERIKALI HAITAVUMILIA WAKANDARASI WAZEMBE - WAZIRI MKUU

*Amtaka Waziri wa Maji avunje mkataba ifikapo Mei 31
*Ni mkandarasi aliyenyang’anywa pasipoti na Rais Magufuli

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitavumilia wakandarasi wasio na uwezo na ambao wanapewa kazi lakini wanashindwa kuzimaliza katika muda uliopangwa.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo, leo (Alhamisi, Machi 30, 2017) wakati akizungumza na watumishi wa Halmamshauri ya Chalinze na wale wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (CHALIWASA) katika ofisi zao, karibu na daraja la mto Wami, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

Alikuwa ameenda kukagua mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji Chalinze na ujenzi wa mfumo wa kusafirisha na kusambaza majisafi pamoja na matenki ya kuhifadhia maji ambao umechukua muda mrefu lakini haujakamilika. Awamu ya kwanza ilianza mwaka Septemba mosi 2001 na kukamilika Desemba mosi 2003.

Amemuagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge ahakikishe kuwa kazi ya ujenzi wa mradi huo inaimarika na kufikia asilimia 80 la sivyo, wakamilishe taratibu za kukatisha mkataba na kutafuta mkandarasi mwingine.

Agizo la Waziri Mkuu linafuatia taarifa aliyopewa kwamba mkandarasi wa mradi huo, Overseas Infrastructure Alliance (OIA) Pvt Ltd ya India alipaswa kumaliza kazi hiyo Februari 22, mwaka huu lakini hadi sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 23 tu.

“Nimeelezwa kwamba mmempatia nyongeza ya siku 100 ambayo inaisha tarehe 31 Mei 2017, kama kazi yake haitakuwa ya kuridhisha na kufikia walau asilimia 80, itabidi Mheshimiwa Waziri uendelee na taratibu zako za kukatisha mkataba, tuanze kutafuta mkandarasi mwingine,” amesema.

“Hii kampuni niliikuta Lindi kwenye mradi mwingine wa maji kama huu. Nilitoa maagizo ya kuharakisha ujenzi ukamilike lakini hawakufanya hivyo hadi Mheshimiwa Rais alipoenda na kuagiza mkandarasi anyang’anywe pasi yake ya kusafiria mpaka atakapomalizia kazi.”

“Kwa kifupi ni kwamba hii kampuni haina uwezo wa kufanya hizi kazi, na ndiyo maana hadi sasa wamekamilisha asilimia 23 tu ya mradi wakati walipaswa kuwa wamemaliza hivi sasa,” amesema Waziri Mkuu na kuongeza: “Mheshimiwa Waziri endelea na utaratibu wa kuwaondoa kisheria sababu hata tukiwaongezea muda bado hawatakamilisha kazi.”

“Nimesikitika sana kukuta mkandarasi hajafikia malengo. Mtu akipewa kazi anapaswa awe na uwezo wa kifedha wa kuifanya ile kazi ili hata Serikali ikichelewesha malipo yake, yeye aendelee na kazi,” ameongeza Waziri Mkuu.

Akizungumzia kuhusu ufanisi wa mradi huo, Waziri Mkuu amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa CHALIWASA, Eng. Christer Mchomba, ahakikishe kuwa wanapeleka maji hadi majumbani mwa wateja na kuweka mita ili wananchi waweze kulipa bili zao badala kuishia kutoa huduma hiyo kwenye vioski (viula).

“Kazi ya kupeleka maji majumbani ni yenu CHALIWASA na siyo ya Wizara. Pelekeni maji na mfunge mita ili watumiaji waweze kulipa bili zao. Pia toeni elimu kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara, waelezeni mipango yenu na wapi mlipofikia. Kazi yenu siyo kutandika mabomba tu, bali kutekeleza majukumu mliyopewa kwa niaba ya Serikali,” amesema.

Kuhusu mitambo inayotumika, Waziri Mkuu amesema mashine zilizopo ni za siku nyingi tangu 2003; hivyo amemuagiza Waziri Lwenge afuatilie upatikanaji wa mashine za kisasa kwani hilo suala ni kubwa na haliwezi kubebwa na CHALIWASA. “Bora mngeanza kuagiza mashine mpya hivi sasa, badala ya kusubiri zichakae kabisa, ndipo muanze kufikiria kuagiza.”

Mapema, akitoa taarifa ya mradi huo, Eng. Mchomba alisema awamu ya tatu ya ujenzi wa mradi huo ilisainiwa Mei 18, 2015 kati ya DAWASA na OIA yenye ubia na kampuni ya Pratibha Industries kutoka India kwa gharama ya dola za Marekani milioni 41.36 ambazo zilikuwa ni fedha za mkopo nafuu kutoka benki ya Exim ya India.

“Kazi zilizopangwa kufanyika ni upanuzi wa mtambo wa maji ili kuongeza uzalishaji wa maji kutoka mita za ujazo 500 hadi 900 kwa siku; ujenzi wa mfumo wa mabomba ya kusambaza maji wenye kilometa 1,022; ujenzi wa matenki makubwa 19 ya kuhifadhia maji; vituo tisa (9) vya kusukumia maji (booster stations) na vioski (viula) vya kuchotea maji 351.”

Alisema hadi sasa mkandarasi huyo amekwishalipwa dola za Marekani milioni 15.81 sawa na asilimia 38 na anaendelea na ulazaji mabomba ambapo hadi sasa amekwishalaza mabomba yenye urefu wa km.141 sawa na asilimia 12.4.

Alisema mradi huo umelenga kuvinufaisha vijiji 68 ambavyo 19 kati ya hivyo viko Kaskazini mwa mto Wami na 49 viko Kusini mwa mto huo.

Akizungumzia utendaji kazi wa mkandarasi huyo, Eng. Mchomba alisema Serikali imechukua hatua za kimkataba dhidi yake kwa kumtoza gharama ya kuchelewa kumaliza mradi (liquidated damages) kuanzia Februari 23, 2017.

“Pia mkandarasi amepewa notisi ya siku 100 ya kumtaka aongeze kasi ya kazi, vinginevyo tutasitisha mkataba ifikapo terehe 31 Mei, 2017 kulingana na kipengele namba 8.7 cha mkataba,” alisema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, MACHI 30, 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages