HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 16, 2017

tiGo kuzindua Usajili vyeti vya kuzaliwa kupitia mfumo wa simu za mkononi

Na mwandishi Wetu

Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo kwa kushirikiana na Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (RITA), pamoja na UNICEF inategemea kuzindua awamu ya nne ya usajili wa watoto chini ya miaka mitano katika mikoa ya Geita na Shinyanga mapema wiki ijayo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na RITA, Mpango huu wa Usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya miaka mitano unatarajiwa kutekelezwa katika wilaya zote tatu (3) zilizo na halmashauri 6 za mkoa wa Shinyanga na Wilaya zote tano (5) zilizo na halmashauri sita (6) katika mkoa wa Geita.
“Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, ni asilimia 9.4 ya watoto wa mkoa wa Shinyanga na asilimia 8.6 katika mkoa wa Geita wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa. Lengo la RITA mara itakapoanza kutekeleza mpango huu ni kusajili watoto wote 740,912 ambao hawajasajiliwa na hawana vyeti vya kuzaliwa katika mikoa yote miwili kwa kipindi cha miezi 6,” alisemakaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Rita Emmy Hudson.
Ili kufanikisha utekelezaji mpango huu kutakuwa na vituo vya usajili zaidi ya 650 vitakavyokuwa na wasajili wasaidizi wapatao 1,250 kwa mikoa yote miwili. Wasajili hawa watawekwa katika ofisi za afisa mtendaji wa mtaa na vile vile katika maeneo ambayo kinamama huenda kupata huduma za kiafya za watoto.
“Matokeo tuliyoyapata mwaka jana katika utekelezaji wa mpango huu katika mikoa ya Iringa na Njombe yatatumika kuhakikisha watoto wote wanapata huduma hii katika mikoa ya Geita na Shinyanga,” alisema Hudson huku akiongeza kwamba mikoa hiyo iliweza kusajili watoto kwa asilimia mia moja (100%) kwa kipindi cha miezi mitano huko Iringa na Njombe.
Meneja wa Huduma za Jamii wa kampuni ya Tigo, Halima Okash alisema kampuni ya Tigo imekuwa mshirika mkuu wa mkakati wa Usajili wa Watoto wa chini ya miaka mitano toka mwaka 2012 ili kuiwezesha serikali kupunguza tatizo la muda mrefu la watoto kutosajiliwa na mamlaka husika pindi wanapozaliwa hivyo kuathiri mipango ya maendeleo ya muda mfupi na ile ya muda mrefu.
“Duniani kote takwimu sahihi na zinazopatikana kwa wakati ni jambo muhimu ili kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo ndio maana kati ya malengo makuu ya mkakati huu ni kutumia teknolojia ya simu za kiganjani katika kuchukua na kutuma taarika kwenda katika kanzidata (database) ya RITA mara mtoto anaposajiliwa kwenye vituo vilivyoaainishwa,” alisema Okash.
Okash aliongeza kwamba kampuni ya simu za mkononi ya Tigo inajivunia kuweza kutumia rasilimali ya ujuzi tulio nao katika kuwezesha kila mtoto nayezaliwa kutambuliwa na mamlaka husika hivyo serikali kufahamu kuna watoto kiasi gani katika umri fulani. 
Cheti cha kuzaliwa ni nyaraka ya awali ya utambulisho kwa mtoto inayomwezesha kutambuliwa uwepo wake na ni haki ya mtoto ya msingi. Hudson aliwaomba wadau wote ikiwa pamoja na viongozi wa mikoa, wilaya, halmashauri, tarafa, kata, mitaa/vijiji na vitongoji kushirikiana kwa pamoja ili kuweza kufanikisha utekelezaji wa mpango huu.
“Vilevile,tunawaomba Viongozi wa dini, wanasiasa, wanahabari na viongozi wa jadi ambao watusaidia kuelimisha wananchi kuhusu kujitokeza kwa wingi kuwasajili watoto ili wapate vyeti vya kuzaliwa,” alisema Hudson.

No comments:

Post a Comment

Pages