HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 14, 2017

Utafiti wa Mafuta na Gesi



Na Talib Ussi, Zanzibar

Kazi ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar imeanza rasmi jana kwa Kampuni ya Bell Geospace Enterprises Limited ya Uingereza kuaza kufanya  utafiti huo kwa niaba ya Kampuni ya Rak Gas ya Ras Khaimah kutoka Dubai.

Akizindua utafiti huo uliofanyika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume jana, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd alisema kwamba utafiti huo unafungua milango katika rasilimali ya Mafuta na Gesi Asilia.

Alisema kwamba  suala la Mafuta na Gesi Asilia sasa linasimamiwa Zanzibar moja kwa moja baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya marekebisho ya Katiba na kuliondoa suala hilo katika orodha ya mambo ya Muungano.

Balozi Seif alisema kazi hiyo ya utafiti wa Mafuta na Gesi Asilia ni hatua muhimu katika uchimbaji wa  Mafuta ambapo inaweza kuchukua miaka mitano kukamilika kwake kwani ni jambo lenye kuhitaji muda, lakini yapo matumaini makubwa ya kufanikiwa kwa suala hilo.

“Tunawaomba wananchi wawe na utulivu, wasiwe na hofu yoyote wakati watakapoiona ndege hii maana itakuwa ikipita pita katika sehemu za bahari na nchi kavu” alisema Balozi Seif.

Alieleza kwamba kwa muda mrefu Serikali imekuwa na mazungumzo na Kampuni ya Rak Gas ya Ras Khaimah ambayo mazungumzo hayo yamezaa matunda ya kuanza kwa kazi ya utafiti ambapo pia Kampuni hiyo imekuwa mshirika wa maendeleo wa Zanzibar.

Kiongozi wa timu ya Watafiti kutoka Kampuni ya Bell Geospace Enterprises Limited ya Uingereza, Stefan Kuna akitoa maelezo mafupi kuhusu kazi ya utafiti huo, alieleza kwamba watatumia muda wa miezi mitatu kufanya utafiti huo Unguja na Pemba.

Mtaalamu huyo alieleza ndege yao ya utafiti itakuwa ikiruka kila siku mapema asubuhi na itakuwa angani kwa muda wa saa sita wakitafiti maeneo yote ya nchi kavu ya Visiwa Zanzibar vikubwa na vidogo pamoja na maeneo ya bahari iliyozunguka Visiwa hivyo.

“Ili tuweze kurekodi taarifa sahihi na zenye ubora, tutaruka chini kabisa kiasi cha mita 120 juu ya ardhi, tunawahakikishia mitambo ya utafiti haina madhara yoyote yale” Alisema Stefan.

Kwa Upande wake menaga wa Uchimbaji mafuta na gesi kutoka kampuni ya RAKGES Dr. Ossama Abdel alieleza kuwa watafanyakazi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu kwa hatua ya awali na katika hatua ya pili watachukua miaka miwili.

“Kama tumejirisha na kugundua basi baada ya miaka miwili tutaaza kuchimba nishati hii ambayo wazanzibar wanahamu nay asana” alieleza Dr. Ossama.

Kiongozi huyo wa timu ya Wataalamu alisema kwamba ndege itaanza kuruka moja kwa moja Kaskazini Kusini ikijumuisha maeneo yote ya Unguja na Pemba na maji yanayozunguka Visiwa hivyo.

Awali , Waziri wa Ardhi, Maji Nishati na Mazingira Zanzibar, Salama Aboud Talib alisema aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano wakati wote wa utafiti na kwamba amewataka wannchi kuondoa hofu.

Kamapuni hiyo ya kigeni inasaidiwa kazi na kampuni ya kizalendo ya Brunswick Zanzibar Limited ambayo inahusika na shughuli za uombaji wa vibali kutoka Serikalini kwa ajili ya ufanikishaji wa kazi ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia hapa Zanzibar.
  
Kuanza kwa kazi ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia kunaanza baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein kutia saini sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia mwezi Novemba mwaka jana.

Waziri Salama alisema kuwa kabla ya kutungwa kwa sheria hiyo, Serikali ilitengeneza Sera ya Mafuta na Gesi Asilia kwa ajili ya kutoa muongozo kwa sekta hii muhimu katika uchumi wa nchi.

Utafiti huo unakuja kutokana na Zanzibar kuruhusiwa kusimamia nishati hizo kupitia sheria ya 2015 kifungu cha 4.

No comments:

Post a Comment

Pages