HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 15, 2017

WANANCHI WATOA MAONI KUELEKEA UCHIMBAJI VISIMA VYA JOTOARDHI MRADI WA NGOZI

Na Johary Kachwamba -TGDC

Wananchi wa Wilaya za Rungwe na Mbeya Vijijini pamoja na wadau wengine wa mradi wa jotoardhi wa Ngozi wametoa maoni mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuuliza maswali ya msingi kabla ya zoezi la uchorongaji visima vya uchunguzi na baadae uvunaji mvuke wa kuzalisha umeme utakaotokana na nishati ya jotoardhi. 

Wananchi walipata fursa ya kutoa maoni yao kati ya tarehe 6 hadi 11 Machi, 2017, wakati timu ya wataalamu wa Mazingira na Jamii kutoka Kampuni ya kuendeleza Jotoardhi Tanzania (TGDC) na TANESCO walipotembelea eneo la mradi, ikiwa ni matakwa ya kisheria ya kushirikisha wadau na jamii itakayopitiwa na mradi husika, wakati wa kufanya tathmini ya athari za mradi katika mazingira na jamii.

Maoni yao ilikuwa ni pamoja na kuiomba Serikali kusimamia taratibu za ajira wakati wa zoezi la uchorongaji visima vya jotoardhi, akizungumza Ndugu Yohana Julius wa Kata ya Swaya Vijijini alisema “wanaomba ajira zisizohitaji ujuzi wapatiwe wakazi wa eneo la mradi ili wanufaike moja kwa moja kwa kujiongezea kipato”.

Bibi Mary Gwamaka alisema “wanaomba mradi huu usiwaache nyuma wakina mama, kwani wanao uwezo wa kufanya kazi mbalimbali, hivyo wanaomba wasibaguliwe”

Akijibu moja ya maswali ya wananchi, Mhandisi wa Mazingira kutoka TANESCO Bw. Fikirini Mtandika alisema sheria na taratibu zote za mazingira zitazingatiwa wakati wote wa utekelezaji wa mradi chini ya usimamizi wa Baraza la Udhibiti na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira.

“TGDC inaandaa mikakati mbalimbali ya kupunguza na kuziondoa kabisa baadhi ya athari za mradi huu katika mazingira yetu” aliongezea Mhandisi Mtandika.

Wananchi wa maeneo yote yanayozunguka mradi wa jotoardhi wa Ngozi wameridhia hatua ya uchorongaji visima vya uchunguzi na baadae uzalishaji umeme na wako tayari kutoa ushirikiano. Kata zinazopitiwa na mradi huu ni Ijombe, Swaya-Mbeya vijijini, Swaya Rungwe na Ndanto.

No comments:

Post a Comment

Pages